|
Wananchi Dar waipinga DAWASA kutaka kuongeza gharama za maji
2008-02-28 17:37:38
Na Usu-Emma Sindila, Jijini
Wananchi Jijini wameijia juu kampuni ya majisafi na majitaka, DAWASA kutokana na hatua yake ya kutaka kupandisha bei ya huduma ya maji.
Wakizungumza kwa jazba wakati wakichangia hoja na kutoa maoni yao mbele ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, EWURA, wananachi hao wamezitaka mamlaka husika kutoruhusu ongezeko la bei ya maji Jijini.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Subira Kibiga, mkazi wa Kigamboni, amesema anaishangaa kampuni hiyo kutaka kuongeza gharama za maji il hali maji yenyewe hayawafikii baadhi ya wateja kama yeye.
Naye Bw. Henry Mrema, mkazi wa Sinza amesema kwa miaka 15 aliyoishi Sinza, hajawahi kuona tone la maji ya bomba.
Kwa sababu hiyo, akasema anashangaa hivi sasa kusikia kuwa kampuni hiyo inataka kupandisha huduma za maji wakati maeneo mengi Jijini hayapati bidhaa hiyo muhimu.
Akijibu hoja hizo, mwakilishi toka DAWASA, Bw. Archardo Mutalemwa, amesema matatizo ya maji katika jiji la Dar ni ya muda mrefu na hii inatokana na miundombinu isiyo imara.
Aidha, amesema nia ya DAWASA ya kuomba kuongeza gharama za maji ni kwa wale wanaopata huduma hiyo ili kuweza kulipia gharama mbalimbali zinazohitajika.
Mbali na wananchi hao kupinga ongezeko hilo la bei, Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma zinazodhibitiwa na EWURA CCC, nalo limepinga vikali ombi hilo la ongezeko la bei na kudai kuwa ongezeko hilo ni kumtwisha mtumiaji mzigo mkubwa.
Akiwasilisha maomi ya baraza hilo, Mwenyekiti wa EWURA CCC, Bw. Jamuda Katma, amesema baraza linaona muundo wa sasa wa huduma za maji Jijini Dar wa kuwa na mwendeshaji yaani DAWASCO na mkodishaji yaani DAWASA, unazidi kumuongezea mtumiaji mzigo kwa kuwa anapaswa kulipia gharama za uendeshaji wa taasisi zote mbili na muundo huo hauleti tija.
Amesema baraza pia halioni sababu ya kuwa na DAWASA kwa sasa kwa kuwa majukumu yake mengi yamekuwa yakipaswa kufanywa na mdhibiti, yaani EWURA.
Aidha, Baraza la Ushauri la Serikali nalo limepinga ongezeko hilo la bei ya maji.
Akiwasilisha maoni ya Baraza hilo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bw. Geoffrey Msella, amesema haoni sababu ya DAWASA kuongeza gharama wakati ina uwezo wa kuongeza mapato yake.
``Idadi ya wenye mita ni asilimia 25 na wengi hupewa ankara zao kwa kukadiria. DAWASA inatakiwa kulipa kipaumbele suala la ufungaji wa mita za maji na pia kutoa bili kwa wakati muafaka,`` akasema.
Aidha, akasema kumekuwa na upotevu mkubwa wa maji katika maeneo mbalimbali tofauti na yale yanayoanza katika chanzo cha maji, hivyo wanatakiwa pia kulishughulikia tatizo hilo.
DAWASA imeomba kuongeza bei ya huduma za majisafi na majitaka asilimia 12.7 na asilimia 28.35.
|