27 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Richmond awafunga midomo vigogo
 
2008-02-27 17:29:48
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Wakati sakata la mkataba `bomu` wa Richmond likizidi kushika kasi, baadhi ya vigogo hivi sasa wanaogopa kulizungumzia kama ugonjwa wa ukoma.

Miongoni mwa vigogo hao ni Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Emmanuel Ole Naiko ambaye juzi alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na sakata hilo, lakini leo alipotakiwa kutoa ufafanuzi mdogo,akageuka bubu.

Katika taarifa yake hiyo ya juzi, Bw. Ole Naiko aliituhumu Kamati ya Bunge kuwa inamwonea kwa vile yeye ni Mmasai, mzaliwa wa Monduli, sawa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa hiyo, Bw. Edward Lowassa.

Hata hivyo madai hayo yamejibiwa na Mjumbe wa kamati hiyo ya Bunge Mheshimiwa Lucas Selelii aliyesema kuwa watuhumiwa wanaoilaumu kamati wanapasswa kujibu hoja badala ya kuituhumu.

Lakini leo, Alasiri ilipomtaka kuzungumzia sakata la Richmond, amegoma akisema hayuko tyari.

``Sitaki kabisa kuzungumzia tena suala la Richmond, maana taarifa yangu nimeshaisambaza kwenye vyombo vya habari, sipendi kuendeleza malumbano na kamati, kama unahitaji kujua zaidi kuhusu Richmond, waombe wenzio taarifa yangu uisome,`` akasema Bw. Ole Naiko.

Alipotakiwa kumtaja mmiliki wa kampuni ya Richmond ambaye ofisi yake ilimpa cheti cha uwekezaji, Bw. Naiko akadai kuwa amemtaja kwenye taarifa yake hiyo kuwa ni Mohamed Gire wa Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Bunge, Mohamed Gire anaelezewa kuwa ni mmiliki wa Kampuni ya kuchapisha vitabu ya nchini Marekani, hivyo mwandishi wa habari hizi alihitaji kujua mwekezaji huyo alikuja kuwekeza nini nchini.

``Waulize Brela (Mamlaka ya Usajili wa makampuni) ndio wanajua kazi ya mwekezaji huyo, maana hata sisi tuliwapa cheti cha uwekezaji baada ya kuwa wamekwishasajiliwa huko,`` akasema Bw. Ole Naiko.

Hata hivyo mwandishi wa habari hizi akataka kujua cheti alichopewa mmiliki huyo wa Richmond kilionyesha anakuja kuwekeza kwenye biashara gani.

Hata hivyo Bw. Naiko akajibu kuwa cheti kinaonyesha aina ya uwekezaji anaotaka kuwekeza lakini hakuwa tayari kutaja aina ya uwekezaji na badala yake akasema haitaji tena kuzungumzia suala hilo.

Bw. Ole Naiko alihusishwa na kashfa hiyo na Kamati Teule ya Bunge kuwa ofisi yake ya TIC ilipindisha taratibu zake ili kumpa mwekezaji huyo cheti cha uwekezaji kirahisi.

  • SOURCE: Alasiri
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.