27 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Unyama!
 
2008-02-27 17:28:00
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili

Mwanamke mmoja mkazi wa Kitunda Jijini Dar es Salaam amenusurika kufa katika kifo cha kikatili, baada ya mume wake kumfumua utumbo kwa kisu kabla ya kumchana chana sehemu mbalimbali mwilini.

Tukio hilo la kinyama, lilitokea majuzi huko Kitunda majira ya saa 3:00 usiku wakati mwanamke huyo Bi. Ustina John, 32, alipokuwa akitoka kwenye biashara yake ya kuuza mchicha jirani na nyumbani kwake.

Hivi sasa Bi. Ustina amelazwa katika taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili, MOI, ambapo madaktari wanajitahidi kumpatia huduma za matibabu kutokana na mwili wake kujaa majeraha ya visu.

Akiongea kwa taabu katika wodi ya Sewahaji, Ustina anasema mtu aliyemfanyia kitendo hicho cha kinyama ni mume wake wa ndoa aliyemtaja kwa jina la John Nyandege, 36.

Akisimulia tukio hilo, amesema matatizo ya mume wake aliyefunga naye ndoa mwaka 1992 huko mkoani Mara, yalianza mapema mwaka huu baada ya bwana huyo kumpata mwanamke mwingine.

Akasema, kutokana na kuchoshwa na tabia hiyo ya mume wake, ambaye kila mara alikuwa akitamka kuwa hamtaki, aliamua kuondoka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi eneo la Kitunda na kwenda kupanga chumba eneo lingine ili aendeshe maisha yake.

``Sikuweza kuvumilia hali ile, kila mara mume wangu aliniambia hanitaki na kibaya zaidi alikuwa na mwanamke pale mtaani, huko ndipo alipokuwa akilala na kufanya kila kitu,`` akasema Bi Ustina.

Akaeleza kuwa ilipofika Februari tatu mwaka huu, mumewe huyo alifika katika chumba alichokuwa akiishi wakati yeye yupo kwenye biashara zake na kuchukua kila kitu na kisha kuondoka navyo.

Anasema kufuatia tukio hilo, aliamua kwenda kituo cha polisi cha Sitakishari kuripoti, ambapo bila ya kuchelewa polisi walimkamata na kumuweka ndani kwa siku mbili.

Siku ya tatu aliachiwa kwa dhamana yenye sharti la kurudisha vitu vyote kwa mkewe.

Hata hivyo, anasema akiwa anasubiri siku ya kurudishiwa vitu vyake, siku ya Jumatano ya wiki iliyopita, Bw. Nyandege alifika tena katika chumba cha mwanamke huyo na kusomba mashuka na nguo zingine na kuzichoma moto huku akitamba kuwa lazima atamuonyesha yeye ni nani na kwamba kitendo chake cha kumpeleka polisi kimechokoza nyuki.

``Nilipeleka tena suala hilo kituo cha polisi cha Sitakishari, kule alileta nguo zingine, mimi nikazikataa kwa kuwa sio zangu, polisi walimwamuru alete zangu siku ya pili yake,`` akasema.

``Lakini ilipofika siku ya Jumatatu usiku wakati nikirudi kununua mchicha wa biashara yangu, nilishtukia mume wangu akitokea mbele na akanivutia kwenye kichaka kilicho jirani na barabara, ambapo huko alianza kunikata kata kwa kisu mwili mzima huku akisema siku hiyo ndiyo ilikuwa siku yangu ya mwisho.

Kana kwamba hiyo haitoshi, mwanamke huyo akadai kuwa, mumewe alichukua kisu na kufyeka vidole vya mkono wa kulia na sehemu nyingine za mwili.

Amesema baada ya kuhakikisha, hana nguvu, mumewe, alichukua kisu na kuanza kumchinja, lakini azma yake hiyo haikufanikiwa baada ya mtu mmoja aliyesikia sauti ya mikoromo ya mwanamke huyo, kusogea karibu na eneo la tukio.

Amesema mtu huyo alipofika kwenye kichaka hicho alishuhudia mwanamume huyo akihangaika kumgeuza shingo mkewe ili amchinje, ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada. Kitendo hicho kilimfanya bwana huyo atoke nduki.

Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa amesema kwa ujumla hali ya Ustina ni mbaya kutokana na visu hivyo kumharibu kwa asilimia kubwa mwilini.

``Tulimpokea akiwa katika hali mbaya, mwili wake wote umekatwa na visu, sehemu ya tumbo imepasuka pamoja na uvimbe uliotokana na kipigwa...hata hivyo tunaendelea kumpatia matibabu,`` akasema Bw. Jumaa.

  • SOURCE: Alasiri
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.