27 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Daladala Jijini yaua wawili, kujeruhi 10
 
2008-02-27 17:26:08
Na Kiyao Hoza, Polisi Kati

Watu wawili wamefariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa vibaya katika ajali ya daladala iliyohusisha magari matatu Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Pius Sheka ameliambia gazeti hili kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 2:00 usiku katika maeneo ya Kimara Suka barabara ya Morogoro.

Amewataja waliofariki kuwa ni dereva wa daladala Gasper Sadala na abiria John Mziray mwenye umri wa kati ya miaka 25 na 30.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Sheka amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari aina ya Scania Tipper lenye namba za Usajili T446 ABW, kushindwa kulimudu gari na kugonga gari jingine.

Amesema dereva huyo Idd Ramadhan, 24, alikuwa akitokea Mbezi kuelekea Kimara na kwamba baada ya kushindwa kulimudu gari lake aliligonga gari aina Volvo lenye namba za usajili T262 ACZ.

Kamanda amefafanua kuwa gari hiyo aina ya Volvo ililigonga daladala Toyota Coaster T 471 AMK lilokuwa likiendeshwa na marehemu Gasper.

Akasema daladala hilo lilikuwa likitokea Ubungo kuelekea Mbezi.

Amewataja waliolazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa ni Geofrey Mizimu,30, Janeth Frenk,26, Uchungu Mohamed,25, Jitihada Yusuph,28, na Rajab Rashid ,35.

Pia akasema miilli ya watu waliofariki imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya taifa ya Muhimbili.

Katika tukio jingine, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Selemani mwenye umri wa kati ya miaka 25-30 ameanguka ghafla na kufariki dunia.

Kamanda Sheka amesema tukio hilo lilitokea jana saa 9:00 mchana huko Tandale kwa Pakacha.

Amesema mtu huyo alikuwa akiugua kifua kikuu na alikuwa akibwia madawa ya kulevya.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.