|
Madiwani Mkuranga watimkia Tanga kujifunza kwa wenzao
2008-02-27 17:23:40
Na Futuna Selemani, Mkuranga
Madiwani wa wilaya ya Mkuranga waliokuwa kwenye ziara ya mafunzo mkoani Tanga wamesema wamejifunza mambo mengi wakati wakiwa huko na kwamba sasa watahamishia maarifa waliyoyapata katika kuufanya mji wao mdogo wa Mkuranga upige hatua zaidi za kimaendeleo.
Mwenyekiti Mtendaji wa Halmashauri ya mji mdogo wa Mkuranga, ambaye ni diwani wa Kata ya Magawa Kisiju, Bw. Juma Abedi, amesema kuwa ujumbe wa madiwani hao umetembelea Tanga, lengo likiwa ni kujifunza, kujionea namna na jinsi ya kuanzisha miji hiyo unavyoendeshwa.
Akasema, wilaya ya Mkuranga ni moja ya wilaya iliyotekeleza agizo la serikali la mwaka 2003, la kuanzisha mji mdogo kila penye makao makuu ya wilaya.
``Ili kukamilisha hilo ndio maana tumekwenda kujifunza kwa wenzetu,``akasema diwani Juma.
Akasema walipokuwa huko walitembelea maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na stendi za magari, masoko na kituo cha redio na luninga cha Tanga.
Pia wakatembelea wilayani Korogwe ambako nako wakaweza kujifunza mambo mbalimbali.
Bw. Juma akasema walipokuwa huko, wamejifunza na kujionea mambo mbalimbali ambayo watayatumia katika kuendeleza miji yao.
Akasema kutembelea katika mikoa mingine ni utaratibu uliopo katika Halmashauri zote ambapo wakati mwingine, madiwani wa mikoa mingine hufika kwao kujifunza.
Aliwataja madiwani wengine aliokwenda nao kuwa ni Bofu wa Kata ya Vikindu, diwani wa Kata ya Mkuranga, Bw. Ali Nangumwa na Mtendaji Mkuu wa Halmashauri hiyo ya mji mdogo wa Mkuranga.
|