|
Mtuhumiwa wa wizi Dar nusra auawe kwa kipigo
2008-02-27 17:22:50
Na Moshi Lusonzo, Jijini
Mkazi mmoja wa Temeke Jijini, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa mahututi baada ya kutuhumiwa kuiba mali za watu na kuishia kula kipigo toka kwa wananchi wenye hasira.
Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI, Bw. Almas Jumaa, hadi sasa, mtu huyo mwanaume bado hajafahamika.
Akasema mtu huyo anakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 25.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mtu huyo alipigwa katika maeneo ya Temeke baada ya kujaribu kuiba kwa mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Katika tukio hilo, wananchi hao walimpiga kichwani kwa kutumia vitu vizito na kumfanya apoteze fahamu ambapo hadi sasa, bado yuko katika hali ya kutojitambua.
Mtu huyo alifikishwa hapo majira ya saa 3:00 usiku juzi, akitokea katika Hospitali ya wilaya ya Temeke .
Katika tukio jingine, mkazi wa Zanzibar Bw. Juma Haji Machano, 26, amelazwa katika hospitali hiyo baada ya kugongwa na gari wakati akivinjari na pikipiki katika mitaa ya mji huo.
Katika tukio hilo, Bw. Machano amevunjika mkono wake wa kulia na hali yake imeelezwa kuwa bado haijawa ya kuridhisha.
Kabla ya kufikishwa Muhimbili, aliwahishwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja ya mjini Zanzibar lakini hali yake ilionekana kuwa mbaya siku hadi siku.
Afisa Uhusiano Bw. Almas akasema wagonjwa wote wamelazwa wodi namba 17 jengo la Sewahaji na madaktari wanaendelea kuwapatia huduma.
|