|
SUMATRA yaanzisha ruti mpya ya daladala za Goba
2008-02-25 17:04:57
Na Mwanaidi Swedi, Jijini
Wamiliki wa mabasi ya abiria al maarufu kama daladala wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuomba kutoa huduma katika ruti mpya zilizoanzishwa pembezoni mwa mji ikiwa ni pamoja na ile ya barabara iendayo Mbezi Juu hadi Goba.
Akizungumza na Alasiri, Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kanda ya Mashariki ya Mamlaka ya Usafiri wa Majini na nchi Kavu nchini, SUMATRA, Bw. Conrad Shio, amesema lengo la kuanzisha ruti hizo ni kutaka kuhakikisha kuwa barabara zote zenye magari ambayo si rasmi na yale ya mizigo yanayogeuzwa kubeba abiria na kujulikana kama `chai-maharage`, yaache kazi hiyo.
Bw.Shio amesema kuwa daladala nyingi ambazo zilikuwa zimepewa leseni wakati wa Mamlaka ya Leseni za Usafirishaji Jijini Dar, na ambazo hazipewi tena ruti kwenda katika ya Jiji, ndiyo zinazopewa kipaumbele kwenda pembezoni mwa mji.
Amesema kuwa katika utaraibu wa kawaida, magari ya mizigo hayaruhusiwi kubeba abiria.
Akaongeza kuwa pamoja na katazao hilo la kisheria, bado barabara ya Goba na nyingine za pembezoni mwa mji zinatumia sana magari ya mizigo kubeba abiria kutokana na ukosefu wa daladala rasmi za kwenda huko .
Aidha, amesema kuwa awali walikuwa wanashindwa kuyaondoa magari hayo kutokana na sababu kuwa hapakuwepo ruti rasmi iliyokuwa imeanzishwa.
``Hivi sasa tunasubiri tupate walau daladala tatu za kuanzia... katika ruti hizo mpya, ipo hiyo ya Goba- Samaki au Goba-Tanki Bovu. Yakianza kazi magari hayo rasmi tutaweza kuyaondoa yale ya mizigo katika kutoa huduma ya usafiri,`` amesema.
Akaongeza kuwa hadi sasa, tayari wameshafanya maandalizi ya mwanzo ikiwa ni pamoja na kupima umbakli halisi wa barabara hizo na hatimaye waweze kupanga nauli zake halali.
|