25 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ulinzi, usimamizi bora waongeza wanyama Mto Wami
 
2008-02-25 17:03:04
Na Sabina Mgellah, PST - Bagamoyo

Kuanzishwa kwa Jumuiya ya WAMIMBIKI katika maeneo ya Mto Wami wilayani hapa kumesaidia kupunguza kasi ya kuuwawa kwa wanyama na hivyo kuweza kuongeza kiwango cha utalii wilayani hapa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali (mstaafu) Serenge Mrengo, wakati akizungumza na PST ofisini kwake.

Bw. Mrengo amesema kuwa hapo awali, kabla ya kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, idadi kubwa ya wanyama ilipotea kutokana na kuwindwa na wananchi na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa wanyama katika maeneo ya vijiji vinavyozunguka Mto Wami.

Mkuu huyo wa wilaya amesema, mara baada ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo, kulikuwepo na ulinzi wa kutosha, hali iliyosaidia kuwepo na ongezeko la wanyama katika kipindi kifupi.

``Pale Mto Wami kulikuwa na viboko na mamba wengi sana. Lakini sasa walikuwa wanapungua siku hadi siku... hivi tunapozungumza wameanza kuongezeka tena baada ya kuwekwa ulinzi,`` akasema Bw. Mrengo.

Amesema kuwa eneo kubwa la hapo Wamimbiki liko ndani ya Bagamoyo na lina jumla ya vijiji 24.

Amefafanua kuwa kati ya vijiji hivyo, vitano viko wilayani Morogoro mkoa wa Morogoro, vijiji 16 viko wilayani Bagamoyo na vijiji vitatu viko wilayani Mvomero, pia Morogoro.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi kusaidiana na jumuiya hiyo, pamoja na vikundi vya ulinzi na usalama katika kutunza hifadhi hiyo ili kuongeza kipato katika sekta ya utalii badala ya kuua wanyama hao.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.