03 May 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Paparazi:Wote hawa wameuawa
 
2007-05-03 18:00:33
Na Mwandishi Maalum

Wakati kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni leo, mauaji ya waandishi wa habari yanazidi kushika kasi huku mapaparazi wasio na hatia wakitolewa roho hivihivi bila huruma.

Takwimu zilizotolewa zinaonyesha zaidi ya waandishi wa habari 170 na wafanyakazi wa vyombo vya habari waliuawa katika kipindi cha mwaka jana tu.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi hiyo inaufanya mwaka huo kuvunja rekodi kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya waandishi waliokatishiwa maisha.

Kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya taasisi ya ``Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka,`` (Reporters without Borders) ya mwaka 2006, katika kipindi cha tangu Januari mwaka huu tu, waandishi sita, pamoja na wasaidizi wanne walitolewa roho bila huruma.

Aidha, ripoti ya kila mwaka inayotolewa na muungano wa vyama vya waandishi wa habari, International Federation of Journalists, inaonyesha hatari kubwa zinazowakabili waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari ulimwenguni kote.

Pia ripoti hizo zinataka haja ya kuboresha heshima kwa uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa waandishi wa habari.

Licha ya mikiki yote wanayokabiliana nayo waandishi, lakini vyombo vya habari bado ni nguzo mhimili muhimu wa demokrasia.

``Hakuna mhimili muhimu zaidi wa demokrasia kuliko vyombo vya habari vilivyo huru na hai`` Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleza Rice alikaririwa akisema hivi karibuni.

Inaelezwa kuwa vyombo vya habari vikiwa kama kiunganishi kati ya viongozi wa nchi na raia wake ni uti wa mgongo wa jamii iliyo wazi.

Taarifa zaidi kuhusiana na suala hilo zinasema jamii za kidemokrasia si kwamba hazina kasoro, lakini zinawajibika, na kubadilishana mawazo ni msingi wa utawala unaowajibika.

Mara nyingi, waandishi wa habari ni wa kwanza kufichua vitendo vya rushwa, kuandika kutoka kwenye msitari wa mbele wa sehemu zenye migogoro, na kuweka wazi makosa ya serikali, inaelezwa.

Kazi hii inahatarisha usalama wa waandishi wa habari, na ni jukumu la serikali na wananchi ulimwenguni kote kutetea usalama wao na wajibu wao muhimu katika jamii iliyo wazi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, nchi kama Marekani huwa inatoa taarifa kuhusu ukiukaji, na pia juu ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari katika ripoti zake za kila mwaka za haki za binadamu katika nchi mbalimbali zinazotolewa na Wizara ya mambo ya Nje (Department of State annual Country Reports on Human Rights).












  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.