|
Uchaguzi CCM, ngumi zatembea
2007-05-03 17:59:38
Na Zainab Kihate, PST - Jijini
Uchaguzi wa viongozi wa nafasi mbalimbali katika Chama tawala CCM Jijini unaendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali huku vituko na vurugu vikitwaa nafasi katika baadhi ya maeneo.
Kule Sinza, kumezuka vurugu kubwa miongoni mwa wanachama wa chama hicho na kuwafanya askari polisi waingilie kati katika kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inaendelea kuwepo.
Tukio hilo linalokwenda kinyume na miiko ya CCM katika kuendesha mambo yake, limetokea pale Sinza C ambapo wanachama kibao walijikuta wakikunjana mashati na kutishia kumwaga damu katika kutetea kile walichodai kuwa ni haki yao kwa mujibu wa mwongozo wa chama.
Mbaya zaidi, kilichowagombanisha wana CCM hao waliokuwa tayari kwa lolote ni juu ya mizengwe inayodaiwa kufanywa baina ya wao wenyewe katika kuandaa orodha sahihi ya wapiga kura.
Vagi lenyewe lililojiri mishale ya saa 6:00 mchana lilikuwa hivi:
Mida hiyo ya sita na dakika kadhaa mchana, taratibu ziliendelea kufanywa katika kukamilisha mchakato huo wa kuchagua viongozi wa tawi la CCM Sinza C.
Wakiwa nje ya ukumbi wa mikutano wa tawi hilo la Sinza C, wanachama waliitwa mmoja mmoja ili kuingia ukumbini na hatimaye kupiga kura.
Mara, msomaji alipomaliza kuwaita waliostahili kupiga kura, wanachama wengine zaidi ya miamoja waliokuwa na kadi zao mkononi wakaanza kupagawa kwa kuona wao wametengwa katika kuwachagua viongozi wanaowataka.
Walipouliza, inasemekana walijibiwa bila maelezo mengi na wasimamizi kuwa majina yao hayamo na hivyo hawataweza kupiga kura.
Hamad! Kitimtim kikaanzia hapo. Wale walioachwa wakaanza kukwidana mashati na wengine katika kutetea kile walichodai kuwa ni haki yao, huku wakihoji ni kwa nini wakatakiwa wapige kura watu 310 tu wakati orodha halisi ilikuwa na majina ya wapiga kura halali zaidi ya 400.
Kelele zikaanza, mitusi mizito ikamwagwa na watu wakaanza kukunjana mashati.
Kwa bahati, kuna mtu alishastukia dalili za kutibuka kwa amani katika eneo hilo na hivyo akawa ameshawatonya polisi.
Dakika si nyingi, askari waliokuwa kamili wa IGP Mwema wakawasili eneo hilo na kufanya vitu vyao, hivyo zile fujo za kumwagiana mitusi na kuanza kukunjana mashati zikaishia hapo.
Wakizungumza na PST kwa nyakati tofauti, baadhi ya wale waliokataliwa kupiga kura wamesema kilichotokea ni kwamba, kuna wasimamizi tawini hapo wamechana majina yao kwa sababu wanazozijua.
``Tumefanyiwa kitu cha ajabu… mimi kwa mfano ni mwanachama wa miaka mingi, tena ni mjumbe. Leo hii nazuiwa kuingia ndani ili kupiga kura, niwaeleweje?`` Akasema mzee mmoja.
Hata hivyo, ilibainika baada ya kuzuka vurugu, viongozi wa tawi hilo waliwasiliana na ‘mabosi’ wao ambapo baadaye, ikatolewa amri kuwa uchaguzi huo uahirishwe hadi utakapotangazwa tena baadaye.
``Tafadhali nifuate baadaye … sina maelezo zaidi kwa sasa,`` akasema Mwenyekiti wa tawi hilo, Bw. Rey Zumba wakati alipotakiwa na mwandishi kueleza zaidi kuhusu kile kilichojiri.
Nafasi zilizokuwa zikigombewa ni ile ya mwenyekiti, katibu mkuu, katibu mwenezi, ujumbe wa wilaya na nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Uchumi na Mipango.
Katika uchaguzi mwingine kama huo Temeke, mgombea mmoja alitoa kali ya mwaka baada ya kujikuta akiangua kilio mbele ya hadhara.
Tukio hilo limetokea pale katika tawi la CCM kata ya 15 ambapo mgombea aitwaye Bw. Ally Mchumira ‘Panya’ alimwaga chozi mbele ya hadhara.
Mgombea huyo wa nafasi ya ukatibu mwenezi, Bw. Ally Mchumira, almaarufu kama Panya, aliangusha kilio hicho kwa sababu ya kile alichosema mwenyewe kwa kinywa chake kuwa eti, nduguye mmoja wa damu alikuwa akimbania.
`Panya` alimuangusha kigogo mwingine waliyekuwa wakiwania nafasi hiyo kwa muda mrefu bila mafanikio, Bw. Fadhil Lupatu.
Ikadaiwa kuwa Bw. Panya alimwaga chozi hilo mara baada ya kutangazwa mshindi na kudai kuwa kilio chake kilitokana na furaha aliyonayo baada ya kushinda kwa mbinde, licha ya kuwa kaka yake alimbania sana na kumwekea kauzibe ili asifurukute katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, Panya hakushinda kirahisi ambapo uchaguzi huo ulirudiwa kwa mara ya pili baada ya wawili hao kwenda sare katika kura za awali na Bw. Lupatu kung`olewa ulingoni.
Wakati mgombea huyo akimwaga chozi, Diwani kiongozi mkongwe wa kata ya Miburani, Bw. Shaaban Mchumila, naye alijikuta akiwa nje ya mchuano huo baada ya kubwagwa na mpinzani wake.
Diwani huyo aliangushwa kwenye mchakato wa kura za maoni za chama hicho wa kuwania udiwani ambapo Bw. Fortunatus Mwang\'wela aliibuka kidedea.
Uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa ofisi za kata hiyo ambapo mwanamama mkongwe, Tatu Juma Farijala, aliibuka kidedea baada ya kumuangusha kigogo Mchumila kwa kishindo.
|