03 May 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wagombea Yombo wadaiwa kupigana juju
 
2007-05-03 17:56:29
Na Onesmo Kapinga, Yombo Kilakala

Waliokuwa wagombea katika uchaguzi wa viongozi wa CCM, tawi la Yombo Kilakala pale Temeke wametoa mpya kwa kila mmoja kuwahofia wenzie kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya tetesi za kupigana juju kutawala.

Vimbwanga hivyo vya kuhofia juju, vilipata nguvu zaidi baada ya wagombea wote kugomea kuingia katika chumba cha uchaguzi, ikidhaniwa kuwa kila mmoja anahofia kufanyiziwa ili asishinde.

Mwandishi alishuhudia wagombea hao wakisitasita pale nje ya ukumbi kwa muda wote ambapo walisimama nje ya ukumbi wa kupigia kura hata pale wafuasi wao walipoanza kueleza misimamo yao ya kiuchaguzi kivitendo katika kupiga kura.

Shughuli zilipoisha huko ndani, ndipo wagombea hao walipokubali kuingia ambapo walipofuatwa na mwandishi ili kujua kulikoni hata wakaogopa kupigwa juju kama ilivyokuwa ikivumishwa na kila mmoja mahala pale, walikataa kuzungumzia.

Hatahivyo, licha ya tetesi za mikwara ya kupigana juju, hatimaye mshindi alipatikana ambapo Bw. Peter Chando alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya kuwabwaga wenzake wawili kwa kura 76.

Wagombea wengine wa nafasi hiyo, Bw. Said Kabalika alipata kura 47 na Bw. Mohamed Kombi kura sita.

Nafasi ya Katibu Mkuu ilikwenda kwa Bw. Juma Ngetabuli na Katibu Mwenezi aliula Bakari Ngurumo.

Katika nafasi ya Uchumi na Mipango ilichukuliwa na Bw. Mkumbia Ngwele na Bi. Maimuna Mpunga alichaguliwa kuwa mjumbe wa tawi wa kuwakilisha wilaya.

Wengine ni Bw. Samson Chacha, Bi. Hawa Hemed, Bw. Hashim Yasin na Bw. Mohamed Barka ambao walichaguliwa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa kata ya Vituka.

Wakati huo huo, Fransisca Jeremiah anaripoti kutoka Tandale uchaguzi wa huko pia ulikumbwa na dhoruba kwani zaidi wanachama 180 wa chama hicho, tawi la Tandale, wamegoma kufanya uchaguzi.

Wanachama hao waligomea kufanya uchaguzi huo, kwa madai kuwa kuna mamluki kibao waliovamia anga zao ili kubadilisha matokeo ya yule anayetakiwa mtaani kwao.

Wakizungumza na Alasiri kwa nyakati tofauti katika eneo hilo la uchaguzi, baadhi ya wanachama walidai kuwa orodha ya majina iliyosomwa sio halali kwa kuwa wengi wao wameshafariki.

Wakasema orodha iliyotumika ni ile iliyoorodheshwa mwaka 2000.
``Orodha ndio kikwazo kikubwa kilichofanya uchaguzi huu ukwame,`` akasema mmoja wa wanachama wa tawi hilo.

Kizazaa kilianza hivi: wanachama wote waliingia ukumbini saa 3.00 asubuhi.

Mjumbe wa kamati ya siasa anaingia na orodha ya majina katika ukumbi huo.

Orodha hiyo inasomwa na kati ya majina hayo, mengi yakabainika kuwa wenyewe wameshafariki dunia.

Kiongozi wa uchaguzi anapomaliza kusoma majina ya wanaotakiwa kuwa katika ukumbi huo, anawataka wasiotajwa katika orodha hiyo kutimua haraka iwezekanavyo.

Wanachama wanagoma hadi waione orodha hiyo huku wengine wakisusa na kurejea majumbani kwaona wengine kudai kuwa wanaogopa kulishwa mboko na mamluki waliofika tawini kwao kwa hamu ili wamchague mtu aliyewakodi!

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.