|
Wajasiriamali kibao Mkuranga walamba mikopo kupitia SACCOS
2007-05-03 17:55:03
Na Humphrey Kadege, Pwani
Zaidi ya wajasiriamali 165 wa vijiji viwili vya wilaya ya Mkuranga mkoani hapa, wamenufaika kupata mkopo wa shilingi milioni 10 uliotolewa kwa ajili ya kujiendeleza kibiashara.
Mikopo hiyo imetolewa na vyama viwili vya kuweka na kukopa, SACCOS vya wilayani humo na kukabidhiwa kwa wajasiriamali hao na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bw. Henry Clemence.
Hundi hiyo ilitolewa na SACCOS za Mwambao na Wananchi baada ya kupokea maombi kutoka kwa wajasiriamali hao.
Bw. Clemence amewataka wafanyabiashara hao kutumia fedha za mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa wana nia kweli ya kujiendeleza ili kuondokana na umasikini.
``Kumbukeni kwamba fedha za mikopo hazitolewi kama zawadi, maana yake ni zitumike kama deni...mkopaji lazima alipe, kwani dawa ya deni ni kulipa,`` akasisitiza.
Akasema tatizo kubwa linalowarudisha nyuma kimaendeleo wafanyabiashara wengi licha ya kukopa kila mara ni kutumia fedha za mikopo kwa malengo yasiyokusudiwa.
DC huyo amewataka wajasiriamali hao kushirikiana na kuwashawishi wananchi wengine kujiunga na vyama hivyo ili kufaidika na mikopo.
Naye Mwenyekiti wa Mwambao SACCOS, Bw. Shukuru Ngw`eshani, alimshukuru DC huyo kwa kuwa NAO pamoja katika muda wote.
Akasema mkuu huyo amewasaidia kimawazo katika changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili na kwamba mafanikio yaliyopatika yanachangiwa na ushirikiano wake.
|