|
`Wasomali huigeuza Bongo kuwa njia ya kutimkia `Sauzi`
2007-05-03 17:54:00
Na Usu-Emma Sindila, Jijini
Imebainika kuwa wahamiaji haramu wanaokamatwa nchini, wakitokea katika nchi za Somalia na Ethiopia, hukimbilia Afrika Kusini na nchi za Ulaya.
Akizungumza na Alasiri ofisini kwake Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Joseph Mungai amesema wakimbizi hao wamekuwa wakikimbia vita vinavyoendelea katika nchi zao.
Amesema kwa sasa nchi ya Somalia imekuwa ikitoa wahamiaji haramu wengi kutokana na vita vinavyoendelea nchini mwao.
``Hawa watu wanapokamatwa, wanahojiwa na vyombo vyetu vya dola na madai yao makubwa ni kuwa wanapita kuelekea Afrika Kusini na hatimaye nchi za magharibi lakini tunawaambia kuwa hii si njia ya kupita,`` akasema.
Amesema wahamiaji hao haramu watapungua endapo amani itapatikana katika nchi ya Somalia na nyinginezo.
Ameongeza kuwa idadi ya wahamiaji haramu waliongia nchini kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2007 toka katika nchi za Somalia na Ethiopia ni 812, ambapo wasomali wakiwa 393 na waethiopia 419.
Aidha amesema idadi hiyo ni kwa wale tu waliokamatwa wakiwa tayari wameshaingia ndani ya mipaka ya Tanzania, ila wapo ambao wamekuwa wakirudishwa makwao wakiwa katika mipaka ya nchi hii.
Mapema mwishoni mwa mwezi jana wahamiaji haramu kutoka Somalia wapatao 99 na wanaosadikika kuwa ni askari walikamatwa eneo la Njombe wakiwa njiani kuelekea nchini Malawi.
|