|
JK alimwa, maisha bora lini?
2007-05-02 18:07:16
Na Sharon Sauwa na Emmanuel Lengwa, Jijini
Siku moja tu baada ya wafanyakazi kumsomea risala yenye kilio cha kutaka mishahara `bomba` na pia kuzungumzia matumizi ya Serikali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Jakaya Kikwete amepewa changamoto nyingine `inayoilima` Serikali yake.
Walioilima Serikali na kutaka irekebishe baadhi ya mambo yake kiutendaji, ni Chama cha Wananchi, CUF, ambao wameiambia Alasiri leo asubuhi kuwa hivi sasa, Serikali imekuwa na matumizi mengi ya kifahari tofauti na hali za wananchi wake.
Naibu Mkurugenzi wa Haki na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Bw. Salum Bimani, amesema licha ya wafanyakazi kuwa na mafao kidogo, bado Serikali ya sasa imekuwa ikifanya baadhi ya matumizi aliyodai kuwa ni ya kujitakia na tena ni mzigo kwa taifa.
Bw. Bimani ambaye alikuwa akizungumzia risala iliyotolewa jana na wafanyakazi kwa rais Kikwete wakati wa kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, amesema Serikali imekuwa ikinunua magari kibao ya bei mbaya na kuwaacha wafanyakazi wakitaabika kimaisha.
Ameongeza kuwa hivi sasa, sherehe za Mei Mosi zimepoteza muelekeo kwa sababu wafanyakazi wanakabiliwa na hali ngumu kimaisha.
Amesema ni vyema sasa kwa wafanyakazi kupewa uhuru wa kutumia silaha yao ya mgomo kila wanapohitaji kuelezea jambo ambalo wamelilalamikia kwa muda mrefu bila ya kupata ufumbuzi.
``CCM itekeleze ahadi zake inazozitoa kila mara... kwa hili la maisha duni kwa Watanzania, inadhihiridha kuwa ahadi zao nyingi ni hewa, na anayezikumbushia anaonekana mbaya ingawa ukweli ni kwamba nyingine hazitekelezeki.`` Akasema Bw. Bimani.
Jana katika sherehe za Mei Mosi zilizoadhimishwa kitaifa huko mkoani Mwanza, wafanyakazi waliilima Serikali ya Rais Kikwete kwa kueleza kuwa baadhi ya matumizi yake yanaonekana kuwa ni ya anasa.
Wafanyakazi hao katika risala yao iliyosomwa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw. Nestory Ngula kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza kuwa hali kwa mfanyakazi wa chini ni ngumu huku Serikali ikifanya matumizi ya anasa, hasa kwa kununua magari mengi ya kifahari, semina za mara kwa mara na misafara mikubwa ya viongozi.
``Serikali ipunguze kununua magari ya kifahari na kufanya misafara mikubwa wakati wa ziara za viongozi… hii itasaidia kubana matumizi ya Serikali na kuboresha maslahi ya wafanyakazi,`` risala hiyo ikasema.
Kana kwamba hiyo haitoshi, wafanyakazi hao walibeba mabango mbalimbali yenye ujumbe tofauti uliokuwa ukimpasha wazi Rais Kikwete kushughulikia matatizo yao.
Baadhi ya mabango hayo yaliandika `Tunataka kima cha chini cha mishahara 350,000`, `Tofauti ya vipato baina ya wageni na wazawa ni ubaguzi, `Serikali iache anasa itujali walalahoi`, na `Tunataka maisha bora kwa kuboresha maslahi yetu`.
Hata hivyo ulipofika wakati wa rais Kikwete kujibu mapigo ya madai ya wafanyakazi hao, hakueleza kile wengi walichokitarajia cha kutangaza kupanda kwa mishahara ya wafanyakazi.
Katika hotuba yake ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na wafanyakazi wengi nchini, rais Kikwete aliwataka wafanyakazi waishi kwa matumaini kwa vile Serikali yao inashughulikia namna ya kuwaborehea maslahi yao.
``Serikali inaendelea kushughulikia namna ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Ntukamazina,`` akasema Rais Kikwete.
|