|
Tandale kufaidi mapesa ya SACCOS mwezi huu
2007-05-02 18:01:46
Na Fransisca Jeremiah na Mariam Mkumbaru, Tandale
Chama cha kuweka na kukopa cha wakazi wa Tandale katika Manispaa ya Kinondoni, Tandale Community SACCOS, kinatarajia kuanza kutoa mikopo kwa wanachama wake mapema mwezi huu.
Diwani wa Kata ya Tandale, Bw. Hamed Mwilima, amesema mpaka sasa wanachama wake wamewekeza zaidi ya Sh. Milioni 3.4 na kwa sababu hiyo, ni wakati muafaka sasa wa kuanza kupata mikopo.
``Mwanzoni mwa Mei tutaanza kutoa pesa hizo kwa wanachama wetu ili waweze kujikwamua kiuchumi,`` akasema Diwani Mwilima ambaye pia ni Naibu Meya wa Jiji.
Bw. Mwilima aliyasema hayo wakati alipohudhuria uchaguzi wa viongozi wapya wa chama chao hicho, ambao ulifanyika katika Shule ya Msingi Tandale.
Katika uchaguzi huo, mgombea Sylvester Ngalaba aliibuka kidedea katika nafasi ya uenyekiti kwa kuzoa kura zote 255 za wajumbe waliopiga kura.
Naye Athumani Magembe alichaguliwa kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wakati Wiliam Chitanda, Rosemary Ngagawa na Muhidini Saidi, wote walichaguliwa kushika nafasi za ujumbe katika kamati ya mikopo.
Uchaguzi huo ulifanyika chini ya usimamizi wa Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Ramadhani Bukuku, ambaye aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa chama chao kinatimiza malengo yake.
Katika hatua nyingine, Bw. Mwilima amejitolea vifaa mbalimbali vya ofisi ya SACCOS hiyo ya Tandale na pia akajiunga na chama hicho.
Aidha, wakazi wa Tandale walimshukuru diwani huyo kwa kuwahamasisha katika maendeleo, hasa kwa kuwaaanzishia SACCOS hiyo.
|