|
Waliovunjiwa mabanda Magomeni walia na Manispaa ya K`ndoni
2007-05-02 18:00:56
Na Valery Kiyungu,Magomeni
Wafanyabiasha 273 wenye umoja uitwao DILOLE pale katika soko la Magomeni Jijini, wameulalamikia uongozi wa Manispaa yao ya Kinondoni wakidai kuwa umeruhusu kuvunjwa kwa mabanda yao ya biashara bila kufuata utaratibu na kufikiria athari zitakazowapata.
Akizungumza na Alasiri, Katibu Mkuu wa kikundi hicho, Bw. Ally Luyaya, amesema mabanda hayo yamevunjwa Aprili 28 mwaka huu, chini ya usimamizi wa uongozi wa Manispaa ya Kinondoni.
Bw. Luyaya alidai uvunjaji huo umewasababishia hasara kubwa.
Akasema wako katika eneo hilo kwa karibu miaka 30 sasa, wakiendesha shughuli zao za kuuza bidhaa na kwamba wameshangazwa na hatua hiyo.
Akasema wafanyabiashara wa kikundi chake, hujishughulisha na uuzaji wa matunda, mbogamboga, nafaka na viazi.
Bw. Luyaya akasema kabla ya kuvunjiwa, uongozi wa manispaa hiyo, ulipanga kuwahamishia ndani ya soko la Magomeni.
Akasema hatua hiyo waliafikiana nayo lakini wakati wakisubiri kutekelezwa, wakashangazwa na hatua ya uongozi huo kuwavunjia ghafla mabanda yao.
Akifafanua, Bw. Luyaya amesema kikundi chake hakipingani na maamuzi ya manispaa ya kuwahamishia ndani ya soko la Magomeni, bali wamesikitishwa na hatua ya kuvunjiwa mabanda wakati ahadi ya kuwagaia nafasi mpya haijatekelezwa.
Aidha, akaiomba Serikali kuingilia kati suala hilo ili lipatiwe ufumbuzi mapema.
Akasema hilo linatokana na shughuli hizo kuwa biashara ndio njia yao pekee ya kujiendeshea maisha yao.
|