|
Magari `vimeo` yaliyotelekezwa kwenye gereji bubu Temeke kupigwa mnada
2007-05-02 18:00:05
Na Futuna Seleman,Temeke
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam, imetishia kuyapiga mnada magari yote yatakayokamatwa katika operesheni ya uondoaji gereji bubu katika manispaa hiyo.
Mwanasheria wa manispaa hiyo, Bw. Greyson Okado, ameyasema hayo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa manispaa hiyo wakati akijibu swali kutoka kwa Diwani wa kata ya Sandali, Bw. Willbroad Tarimo.
Diwani Tarimo alitaka kujua magari yatakayokamatwa katika operesheni hiyo, yatashikiliwa kwa muda gani ili kusiwe na uvunjaji wa sheria.
Akijibu swali hilo, mwanasheria huyo akasema magari hayo yanatakiwa kunadiwa baada ya miezi mitatu toka siku yalipokamatwa.
``Sheria inaruhusu magari yapigwe mnada, lakini haishauriwi sana lifanyike hilo sababu hili huleta matatizo makubwa,`` akasema mwanasheria huyo bila kufafanua zaidi.
Kwa upande mwingine. Alasiri lilishuhudia gari la matangazo la manispaa hiyo likipita kila mtaa kuwatangazia wenye gereji hizo, kuondoa magari yao kabla hatua zaidi9 hazijachukuliwa.
``Tunawatangazia kuwa, baada ya siku tano kila mtu awe ameondoa magari yake katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Vinginevyo yatakamatwa na kuhifadhiwa katika yadi ya Manispaa kabla ya kupigwa mnada,`` likasema tangazo mojawapo.
Hivi karibuni, halmashauri hiyo ilitangaza operesheni maalum ya kuondoa gereji bubu zilizopo ndani ya manispaa hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bw. Idd Nyundo, alikaririwa akisema kuwa zoezi hilo la kusambaratisha gereji bubu ni moja ya mikakati ya uboreshaji wa mazingira katika manispaa hiyo.
Alisema zoezi hilo pia litakwenda sambamba na agizo lililotolewa na Serikali kupitia Waziri Mkuu hivi karibuni, lililotaka manispaa kuondoa gereji bubu, kupanda miti na kuboresha mazingira ya Jiji.
|