|
Jk, zigo hiloo!!!
2007-05-01 17:34:37
Na Waandishi Wetu Dar na Mwanza
Majiji ya Dar es Salaam na Mwanza leo yamefurika maelfu ya Watanzania waliojitokeza kwenye maadhimisho ya sherehe za Wafanyakazi Duniani almaafuru kama Mei Mosi.
Huko Mwanza, maelfu hayo yameongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Jakaya Kikwete wakati hapa Jijini kinara alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bwana Abbas Kandoro.
Alasiri iliyodamkia kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini yalikofanyika maadhimisho hayo, imeshuhudia wananchi kibao wakiwa wamefurika kwenye viwanja hivyo.
Wafanyakazi waliotinga sare za kupendeza huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali waliandamana kutoka maeneo ya BIT hadi viwanjani hapo ambapo walipokelewa na Mkuu wa Mkoa.
Miongoni mwa ujumbe ulioandikwa kwenye mabango hayo ni ``Mishahara iende sawa na mfumuko wa bei`` na ``Hali bora zitaongeza ari ya kazi`` na ``Ubaguzi katika maslahi unachochea vurugu``.
Mengine yameandikwa, ``Kandoro dhibiti msongamano wa magari, watu wawahi kazini``, ``Serikali iwe macho na wawekezaji wababaishaji``.
Kwa upande wa Mwanza ambako sherehe hizo zinafanyika kitaifa, maandamano yalianzia katika Ofisi za Chama cha wafanyakazi,TUCTA, zilizopo jirani na Uwanja wa Nyamagana, katikati ya Jiji la Mwanza hadi Uwanja wa CCM Kirumba ambako Rais Kikwete ameyapokea.
Rais Kikwete amewasili kwenye uwanja wa CCM Kirumba mishale ya saa 4:25 asubuhi akiwa na mkewe Mama Salma Kikwete na kuanza kupokea vikundi mbalimbali vya wafanyakazi vilivyoanza maandamano tangu saa 1:30 asubuhi.
Timu ya Rais Kikwete Jijini Mwanza inao pia Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Kapteni (Mstaafu) John Chiligati, Waziri wa Kilimo na Chakula, Bw. Steven Wasira, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Bw. Antony Diallo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,TAMISEMI, Bw. Mizengo Pinda.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Lawlence Masha.
Baada ya sherehe za Mei Mosi, Rais Kikwete atafanya ziara ya siku kumi kutembelea maeneo mbalimbali.
Mkoa wa mwanza umejawa na shamrashamra kubwa juu ya sherehe hizo, huku wafanyakazi wengi wakiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua viwango vipya vya mishahara.
Wakati tunakwenda mitamboni, taarifa kutoka viwanja vya Mnazi Mmoja zimesema mvua kubwa imetibua sherehe hizo, hali iliyowafanya wananchi waliohudhuria, kuvamia jukwaa la mgeni rasmi, mzee mzima Kandoro.
|