|
Sada achangiwa zaidi
2007-05-01 17:29:42
Na Mwandishi Wetu, Mikocheni
Wakati mtoto Sada Mwesi ambaye alizaliwa bila pua akiendelea kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jengo jipya la IPPM kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya yake kabla ya kuanza kutibiwa, wasamaria wema zaidi wamejitokeza kumsaidia.
Baada ya kuwa tayari ameshatoa Sh. 100,000, mwanafunzi Angel Mgewa wa kidato cha tatu katika Shule ya Good Samaritan ya Jijini, ameahidi kujibana zaidi matumizi yake ya shule ili awe akimchangia Sada Sh. 10,000 kila mwezi.
``Amenigusa kwakweli... Mungu akiniwezesha, nitaanza kutekeleza ahadi yangu hii kuanzia mwishoni mwa mwezi ujao (Mei),`` akasema Angel aliyekuwa ameongozana na mwenzie kwenye ofisi za gazeti hili.
Mwingine, ambaye awali alichangia Sh. 50,000, ni Mama Mrema wa Mbezi Jijini. Yeye ameongezea Sh.200,000 zaidi katika mchango wake wa awali, hivyo kutoa jumla ya Sh.250,000 kwa ajili ya mtoto Sada.
Pia, Watanzania wawili, mmoja anayeishi nchini Uingereza na mwingine wa Italia, kwa nyakati tofauti jana walituma taarifa kuwa tayari wameshatuma michango yao kwa Sada na Alasiri itafuatilia.
Mama wa mtoto huyo, Bi. Mwanaidi Mwesi, 17, ambaye alifika katika ofisi za gazeti hili kuomba msaada wa kuchangiwa pesa za kugharamia matibabu hayo, amesema madaktari wa Muhimbili wameshauri alazwe ili iwe rahisi kuchunguzwa na tayari mtoto huyo amelazwa.
Kabla ya hapo, mtoto huyo alipelekwa katika Hospitali ya CCBRT ambako madaktari walishauri awahishwe Muhimbili.
|