|
Wanaowanga Sinza watajwa hadharani
2006-07-24 15:37:18
Na Mwandishi wetu, Sinza
Wakazi wa mtaa wa Sigara Sinza, Jijini Dar es Salaam, majuzi walijikuta wakikumbwa na mshangao baada ya bibi mmoja anayedaiwa kuwa mwanga kutaja watu 11 aliodai kushirikiana nao katika shughuli za kichawi.
Walioshuhudia tukio hilo wameiambia Alasiri kuwa sakata hilo lilianza majira ya saa 3:00 asubuhi ambapo bibi huyo waliyemtaja kwa jina la Sinahamu Nassoro, 75, alianza kupiga makelele huku akitaja majina ya watu ambao alidai ni wachawi wenzake.
Wakasema licha ya kutaja wanga wenzake pia alitaja baadhi ya marehemu ambao alidai vifo vyao vilisababishwa na kundi lao la kichawi.
Mmoja wa mashuhuda hao akasema mtaa huo wa Sigara sasa umechafuka baada ya orodha ndefu ya watu kutajwa na bibi huyo akisema ni wachawi.
Kila mtu ana hofu. Bibi alitaja watu 11 wote kutoka mtaa huu akisema ni wachawi, mkazi mmoja wa eneo hilo aliliambia gazeti hili.
Akasema miongoni mwa waliotajwa yumo mwalimu mmoja wa shule ya msingi (Jina na shule anayofundisha tunavihifadhi), ambaye anaishi mtaani hapo.
Akasema pia imewasikitisha kusikia watu wawili waliotajwa kuwa wameuawa na kundi hilo la wanga wanawafahamu na ni ndugu zake bibi huyo.
Ingawa watu aliowataja kuwa wamewaua ni ndugu zake mwenyewe lakini imetusikitisha sana kwa vile watu hao tunawafahamu na tuliishi nao hapa wakiwa watu wema sana, akasema shuhuda mwingine.
Watu waliozungumza na Alasiri wameeleza kusikitishwa kwao na kitendo cha bibi huyo ambaye wanasema wamemzoea na hana makuu na mtu yeyote.
Kwa kweli mimi nimeshangaa sana kwani bibi huyu ni mpole , tumemzoea na huwezi kumdhania kuwa ni mwanga, kweli nimeamini huwezi kumjua mchawi kwa macho mpaka aamue mwenyewe kama huyu bibi alivyojidhihirisha leo, akasema mama mmoja anayeishi jirani na nyumbani kwa bibi huyo.
Mpaka Alasiri inaondoka eneo la tukio bibi huyo alikuwa amefungiwa ndani ya chumba maalum na wazee waliokuwa wanalinda chumba hicho walikuwa wakali kama pilipili wakikataza mtu yeyote kuingia ndani ya nyumba hiyo.
Baada ya wazee hao kuweka ngumu kumwona bibi huyo, watu waliokuwa wamefurika kwenye viwanja vya Sigara ambavyo viko mkabala na nyumba anayoishi bibi huyo walianza kuondoka taratibu huk kila mmoja akizungumzia mkasa huo wa aina yake.
Habari za ndani kutoka kwa ndugu wa karibu wa kikongwe huyo zimedai kuwa bibi huyo anaishi na watoto wa marehemu kaka yake baada ya yeye kutojaaliwa kupata mtoto.
Hadi Alasiri inaondoka kutoka kwenye tukio hilo bibi huyo alikuwa bado amefungiwa ndani ili kuepusha watu wasimshushie kipigo.
|