|
Wezi kupitia mtandao watua Jijini Dar es Salaam
2006-07-24 15:36:35
Na Haji Mbaruku, Jijini
Wizi kupitia njia ya teknolojia ya mtandao ambao umekuwa ukifanyika nchi za nje hasa za Afrika Magharibi sasa umetinga Jijini Dar es Salaam na mtu mmoja amefanikiwa kuchota mapesa kwa mtindo huo haramu.
Mtu huyo alifanikiwa kuchota mapesa hayo baada ya kufanya mawasiliano ya muda mrefu na Mtanzania mmoja aishie Marekani akijitambulisha kwa jina feki.
Hata hivyo tapeli huyo alinaswa Jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa kwenye vyombo vya sheria.
Sakata lenyewe liko hivi:Mshitakiwa Emmanuel Salehe, akiwa Jijini Dar es Salaam alifanikiwa kupata anuani ya barua pepe ya Mtanzania mmoja aishie nchini Marekani ambaye ana ndugu yake hapa Dar .
Baada ya kunyaka anuani hiyo aligushi baadhi ya vitu na kisha kuanza kuwasiliana na Mtanzania huyo akijifanya nduguye aishie Jijini.
Baada ya kufanya mawasiliano ya hapa na pale, hatimaye akamchomekea Mtanzania huyo suala la kuhitaji mapesa kiasi cha shilingi milioni 1.5.
Mtanzania huyo wa majuu kwa kudhani ndugu yake ana shida akamtumia pesa hizo bila hiana.
Hata hivyo dili lilifichuka baada ya ndugu huyo wa Bongo kubaini jamaa yake wa Marekani katapeliwa na ndipo alipotoa taarifa vyombo husika na uchunguzi kuanza.
Baadaye tapeli huyo alinaswa na kupelekwa polisi na baadaye mahakamani.
Kesi hiyo ilifikishwa katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu na baada ya kusikilizwa, mshtakiwa akapatikana na hatia na kulimwa kifungo cha miaka kumi jela.
Hata hivyo katika utetezi wake, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa ameshajifunza vya kutosha na sasa anajutia makosa yake.
Ninatambua makosa niliyoyafanya mheshimiwa, nakiri kuwa nilifanya makosa makubwa sana na sasa sitorudia tena kufanya vitendo hivyo, akasema mshtakiwa huyo baada ya mahakama kumtaka ajitetee kwanini asilambishwe adhabu kali kwa kuhusika na utapeli huo.
Licha ya utetezi huo, Hakimu Euphimia Mingi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alimlambisha kibano cha kwenda jela miaka kumi.
Awali, mshtakiwa Emmanuel alidaiwa kuwa siku ya tukio aliwasiliana na dada wa mlalamikaji kwa kutumia barua pepe na kuomba amtumie pesa, na dada huyo akidhania anawasiliana na mdogo wake akatuma pesa hizo.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa aliendelea kuwasiliana na dada yake mlalamikaji na kwa vile alikuwa anajua barua pepe ya mlalamikaji na hata password yake, kazi ya udanganyifu ilikuwa rahisi kwake, akatengeneza kitambulisho cha benki na taratibu zote ili aweze kuvuna asichopanda.
Hata hivyo, baadaye licha ya kwamba alifanikiwa kuzipata pesa hizo, alikuja kukamatwa kufuatia uchunguzi mkali uliofanywa.
Hakimu Mingi wakati akisoma hukumu hiyo alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka na hakuwa na sababu ya kumuachia mshtakiwa huyo.
Kwa upande wa Mwendesha mashtaka wa polisi, yeye aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kwa vile ametumia teknolojia ya kisasa katika kurudisha nyuma maendeleo ya watu nchini.
Mheshimiwa hakimu, matumizi ya teknolojia ya kisasa yaani kompyuta yameletwa nchini kwa minajili ya kurahisisha shughuli za maendeleo, wala hayakuletwa nchini kwa ajili ya kudhulumu watu, naomba mahakama yako itoe adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo, akasema mwendesha mashtaka huyo.
|