24 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Polisi Dar wamwaga risasi kwenye bar
 
2006-07-24 15:35:39
Na Mwandishi Wetu, Kiburugwa

Raia waliokuwa wakiangalia video kwenye bar moja Jijini Dar es Salaam, wamejeruhiwa baada ya kukanyagana wakati wakitimua mbio kuokoa maisha yao kufuatia polisi kumwaga risasi eneo hilo.

Tukio hilo lilitokea juzi usiku saa 2:30 kwenye bar moja ijulikanayo kama Corner Bar iliyoko Mbagala Kiburugwa .

Walioshuhudia tukio hilo wanasema polisi hao waliokuwa kwenye gari lao baada ya kushuka kwenye bar hiyo, walianza kuchukua nafasi na punde si punde mmoja wao akafyatua risasi.

Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo wamesema watu waliokuwa wakitazama video jirani na bar hiyo walitimua mbio huku wengine wakikanyagana na kuangushana, kitendo kilichopelekea baadhi kujeruhiwa.

Baadhi walisikika wakipiga kelele wakisema, ’’tumevamiwa tumevamiwa’’.

Wakati hao waliokuwa kwenye bar wakitimka, huko barabarani nako mambo hayakuwa shwari kwani watu walikimbia ovyo na wenye maduka nao kuyafunga na kutafuta pa kujificha.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, Polisi hao walikwenda ndani ya bar na kukuta vijana wakicheza pool ambapo mmoja wao alianza kuwafokea akisema ”kwanini mnacheza pool wakati imepigwa marufuku?” shuhuda wetu akasema.

Hata hivyo shuhuda huyo amesema hapakuwa na tukio lolote la kihalifu kwenye eneo lao ukiachilia mbali polisi kuhoji vijana hao kwanini walikuwa wakicheza pool na kisha kuondoka nao kwenda kusikojulikana.

Habari zaidi zinasema vijana waliochukuliwa na polisi waliachiwa baadaye usiku huo ingawa haikuweza kufahamika mara moja waliachiwa kwa misingi ipi au kukamatwa kwao kulitokana na nini.

Wiki iliyopita msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi, Isaka Mugasa, alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Said Mwema, amepiga marufuku mchezo wa pool saa za kazi.

Hata hivyo wachunguzi wa mambo wameliambia Alasiri kuwa, tangazo hilo bado halijawafikia watu inavyostahili kwa vile mchezo huo haujazuiwa kuchezwa baada ya kazi.

Hali kadhalika wananchi hao wamesema polisi wasio waaminifu wanatumia tangazo hilo kunyanyasa raia wanaokutwa wakicheza pool hata baada ya kazi.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.