|
Machinga nusra wamtoe roho askari wa Jiji
2006-07-24 15:32:16
Na Margareth Simba, Mwenge
Askari wa usalama barabarani aliyekuwa akiongoza magari eneo la Mwenge, karibu na wachonga vinyago alijikuta akiweka kibarua chake pembeni na kwenda kumwokoa askari wa Jiji aliyekuwa akipokea kibano cha nguvu kutoka kwa Machinga.
Tukio hilo lilosababisha fujo na baadhi ya vibanda vya wauza vinyago kufungwa kwa muda, lilitokea hivi karibuni pale Mwenge kwa wachonga vinyago.
Askari huyo aliyenusurika kuuawa, ametambulika kwa jina moja Felix.
Chanzo cha kuangushiwa kibano ni kitendo chake cha kuwazuia wateja kuingia kwenye duka.
Akisimulia mkasa huo Mwenyekiti Msaidizi wa Wauza Vinyago katika eneo hilo, Bw. Emmanuel Ukoti, amesema siku ya tukio yeye hakuwepo lakini alipewa taarifa na Mwenyekiti wake.
Akasema alielezwa kuwa kulitokea fujo kubwa zilisababisha Felix kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili.
Mwenyekiti huyo akasema baadhi ya wafanyabishara wanaochonga vinyago katika sehemu hiyo waliamua kumkomesha askari huyo kwa vile amekuwa na tabia mbaya ya kuwakataza wateja kuingia katika maduka na kuwalazimamisha kununua bidhaa za wachongaji wa nje kwa kuwaambia kuwa za dukani zinaziuzwa kwa bei ya juu sana.
Kutokana na hali hiyo tulikaa viongozi na kuwashirikisha wauza vinyago...tukaweka askari hawa ili wakikishe kila mteja anayefika hapa awe anaingia dukani, akasema.
Akasema siku ya tukio, askari huyo alileta za kuleta, kitendo kilichowaudhi na kuanza kumpiga.
Kama siyo askari kumwokoa wangemuua, akasema.
Akasema askari wa usalama aliweza kumuokoa kijana huyo ambaye alishazidiwa nguvu na kubaki akitambaa chini huku wamachinga wakiendelea kumpiga kwa mawe na mateke.
Amepigwa sana walikuwa wanamrushia mawe kama mwizi ....nasikia Mwenyekiti alimpeleka polisi Mabatini na hadi leo hii hajatokea kazini kwa sababu ameumia sana, akasema.
Aidha amefafanua kwamba toka kuletwa kwa askari hao Wamachinga wamekuwa wakiwatishia maisha kwa madai kwamba wanawaharibia biashara.
|