24 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wataka kujua biashara isiyolaza mtu njaa?
 
2006-07-24 15:31:03
Na Abdul Mitumba, Manzese Argentina

Ingawa uuzaji ni majeneza ni biashara isiyo na watu wengi lakini waliojikita kwenye shughuli hiyo wanasema ’ukiwa muuza majeneza, kamwe huwezi kulala njaa”.

Wamesema kutokana na ’kutoka’ kwa biashara hiyo, hivi sasa watu wanadiriki kwenda kuweka oda ya kutengenezewa jeneza hata kabla mtu anayeugua hajafa.

Si hivyo tu, imeelezwa kuwa kutokana na ajali za mara kwa mara na ugonjwa hatari wa ukimwi, kuna wakati majeneza katika eneo hilo hununuliwa yote kiasi cha wateja wengine hukosa au kulazimika kusubiri kwa siku moja hadi mbili, licha ya kwamba nyumbani kuna msiba.

Siri hizo zimefichuliwa na mafundi na wauzaji wa majeneza wa pale Manzese hao wakati walipozungumza na Alasiri iliyotembelea katika eneo hilo.

Bwana Cosmas Kobero mmoja kati ya mafundi wa majeneza ameiambia Alasiri kuwa haijawahi kutokea biashara ya majeneza ikawa mbaya.

”Tumekuwa tukiuza majeneza kati ya 60 hadi 100 kwa mwezi hapa, biashara hii imekuwa ya kudumu kwa sababu inahusisha moja maisha ya watu ya kila siku,’’ akasema Bwana Hurbath Daud maarufu kama Nguvumali.

Bwana Nguvumali ambaye anamiliki duka la majeneza amesema kwa wastani jeneza moja huuzwa kati ya Sh.60,000 na Sh.170,000 kutegemea ukubwa na vitu vya thamani vilivyowekwa katika jeneza kwa ajili ya kupamba maiti.

Hata hivyo, akizungumza na Alasiri muuzaji mwingine wa majeneza, Bwana Chatta Seif alisema sehemu kubwa ya biashara hiyo ni huduma.

”Kuna wakati watu wanakuja hapa wakiwa na pesa kidogo na wewe kama binadamu unalazimika kuwapunguzia,’’ akasema.

Amesema katika hali kama hiyo, huwezi kumnyima mtu jeneza eti kwa sababu tu amekuja na pesa isiyolingana na bei iliyopangwa.

”Wajua leo kwa mwenzako kesho kwako au kwa ndugu yako wa karibu, kila mtu atakufa,” alisisitiza Bw.Seif.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.