|
Watoto yatima wasaidiwa
2006-07-24 15:29:32
Na Mary Wejja,Magomeni
Watoto yatima 45 wa tarafa ya Magomeni wamepatiwa msaada wa vifaa vya shule vyenye thamani ya zaidi ya shilingi laki sita.
Msaada huo umetolewa na shirika lisilo la kiserikali la Youth Life Relief Foundation (YLRF).
Mkurugenzi Mtendaji wa YLRF Bw.Khatibu Kunga amesema walionufaika na msaada huo ni yatima kutoka shule mbalimbali za msingi zilizopo katika kata za Makurumla,Ndugumbi na Manzese.
Akikabidhi misaada hiyo, Afisa Maendeleo ya jamii wa manispaa ya Kinondoni na Mratibu wa UKIMWI wa Wilaya hiyo, Bi.Sixtha Komba ametoa changamoto kwa walezi wa yatima hao kutobweteka kwa kusubiri misaada badala ya kuwanunulia vifaa vya shule watoto hao.
Sare ya shule ikichanika mnunulie mwanao sio usubiri hadi apewe msaada na wasamaria, akasema.
Aidha amewataka walezi hao kutokuwa na ubaguzi katika malezi ya watoto hao na kuwachukulia kama watoto wao kwani, kitendo cha watoto hao kupoteza wazazi ni pigo kubwa kwao hivyo wasiwaongezee machungu.
Akasema kuwa ongezeko la mashirika binafsi ya kusaidia yatima hapa nchini linachangiwa na walezi wa yatima kutokuwa na upendo kwa yatima hao kwa kuwalea kama watoto wao ambao uishia kulelewa katika makambi.
Shirika hilo pia hujishughurisha na kutoa mikopo kwa wajane kusaidia yatima kwa ufadhili kutoka Mtandao wa African Community uliopo nchini U.K.
|