|
Majambazi yavamia mahakama
2006-07-21 14:52:10
Na Devota Kabuta, Jijini
Watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi huku moja limetinga sare za kipolisi, wamevamia jengo la Mahakama moja Jijini.
Watu hao walivamia mahakama ya mwanzo ya Manzese Jijini usiku wa kuamkia leo.
Imeelezwa kuwa watu hao walifanikiwa kutinga ndani ya uzio baada ya kuruka ukuta kijinja.
Hata hivyo habari zimesema majambazi hayo kabla hayajatekeleza azma yake, yalikumbana na mlinzi aliyetajwa kwa jina la Faustin Mnungulile ambaye aliyatoa nduki.
Imedaiwa kuwa, katika purukushani hizo jambazi ambalo lilikuwa limevaa magwanda ya kipolisi lilidondosha kofia ya na ikaokotwa na mlinzi huyo.
Tukio hilo linadaiwa kutokea saa 5:30 usiku katika jengo la Mahakama hiyo lililoko maeneo ya Manzese mtaa wa Ukombozi, Jijini.
Imedaiwa kuwa, baada ya majambazi hayo kuruka ukuta wa jengo hilo mlinzi aliyavamia na katika purukushani majambazi hayo yalizidiwa nguvu na kuamua kutimua mbio.
Imedaiwa kuwa, baada ya majambazi hayo kutimua mbio mlinzi huyo alipiga filimbi na majirani wa eneo hilo wakatoka lakini hawakufanikiwa kuyakamata.
Mlinzi huyo amesema majambazi hayo yalikuwa na kamba za katani, matambala pamoja na plasta.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bi. Mariamu Masamalo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema taarifa hizo alizipata saa 6:00 usiku baada ya kutumiwa meseji.
Amedai kuwa, taarifa za tukio hilo ameshamfahamisha bosi wake na amewaagiza walinzi kuingia wawili wawili zamu ya usiku.
Hii ni hatari kama mlinzi huyo angekuwa mzembe wangemuumiza...nimeshamtaarifu bosi wangu na nimewaambia wawe wanaingia usiku walinzi wawili tusije tukakuta maiti, akasema mheshimiwa Masamalo.
Amesema kukosekana kwa umeme kwenye jengo hilo ndiyo sababu inayochangia kutokea kwa matukio kama hayo.
Habari kutoka ndani ya mahakama hiyo zimedai kuwa huenda majambazi hayo yalivamia mahakama baada ya kusikia kuna Sh. Mil. 10 za mauzo ya nyumba ya shauri moja la mirathi.
Kuna nyumba jana iliuzwa kwenye shauri la mirathi Sh. Mil. 10, huenda majambazi hayo yalipata taarifa na yakadhani pesa hizo zipo hapa mahakamani, akasema mfanyakazi mmoja wa mahakama hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Tukio hilo limeripotiwa katika kituo cha polisi cha Urafiki na kufunguliwa jalada namba URP/RP 7571/06.
Askari mmoja wa kituo hicho aliyekuwa zamu ameliambia gazeti hili kuwa mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.
Amesema askari wa zamu kituoni hapo wanaozunguka na gari la polisi la kituo hicho aina ya Defender walikwenda kukagua eneo la tukio na kurudi na kofia hiyo ya polisi iliyodondoshwa na jambazi.
Amesema hakuna mahali popote kulikovunjwa wala kuibiwa kitu katika tukio.
Tangu mwaka huu uanze hii ni mara ya pili kwa jengo hilo kuvamiwa ambapo mwezi mmoja kabla ya tukio hilo kutokea mahakama hiyo ilivamiwa na watu wasiojulikana kwa kuruka ukuta na kutaka kuiba lakini mlinzi akawakurupusha na kuwakamata.
Watu hao hivi sasa kesi yao inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.
Tukio jingine kama hilo liliwahi kutokea mwishoni mwa mwaka jana ambapo watu wasiojulikana walivamia mahakama hiyo na kuvunja ofisi ya mtunza fedha na kuiba cheki za mashauri ya mirathi zenye thamani ya mamilioni ya pesa pamoja na vielelezo mbalimbali vya kesi za jinai.
|