|
Tobaa! Kifo chini ya Fuso
2006-07-21 14:51:19
Na Jimmy Mfuru,Gerezani
Mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Mbaraka Jamali maarufu kama Muba amekufa kifo cha kutatanisha.
Mwili wake umekutwa chini ya uvungu wa gari aina ya Isuzu huku shingoni ukiwa umezungushiwa waya za taa za lori hilo.
Tukio hilo la aina yake limetokea usiku wa kuamkia leo katika mtaa wa Mbaruku, Gerezani huko Kariakoo.
Baadhi ya watu wanasema inashangaza kwani ni vigumu kwa mtu kuingia chini ya fuso na kujinyonga.
Wapo wanaodai kuwa huenda jamaa huyo ameuawa sehemu nyingine halafu mwili wake ukaletwa hapo na kuwekwa waya hizo kupoteza watu maboya.
Huwezi amini Muba tulikuwa naye jana jioni , hata hivyo mazingira ya kujinyonga chini ya lori kwa kutumia nyaya za taa za lori hili yanatupa wasiwasi, amesikika akisema kijana mmoja katika eneo la tukio.
Kwa mujibu wa mjomba wa marehemu, Bw.Yusuf Ayubu marehemu alikuwa na umri wa miaka 38 na kabila lake ni Mmakonde.
Amesema hapa mjini hakuwa na kazi yoyote maalum, kitu kinachomfanya aamini kwamba amejinyonga kutokana na kuzidiwa na ugumu wa maisha.
Gazeti hili leo asubuhi limeshuhudia mwili wa kijana huyo ukiwa bado chini ya lori hilo lenye namba za usajili T758 AJD huku nyaya za taa alizojinyongea zikiwa zinaninginia shingoni. Mwili wake ulikuwa umefunikwa kwa shuka jeupe.
Mwanzoni tulidhani amejipumzisha lakini tulipoona hajitikisi, tukamtafuta mjomba wake ambaye anakaa jirani na hapa, akasema kijana mmoja ambaye hakutaja jina lake.
Leo asubuhi mtaa huo ulikuwa umefurika watu mbalimbali kuangalia tukio hilo ambapo wengi walionyesha wasiwasi juu ya mazingira ya tukio zima.
|