21 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kontena la bidhaa feki ladakwa bandarini Dar
 
2006-07-21 14:48:18
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Tume ya Ushindani wa Biashara nchini, FCC, imekamata kontena moja lenye bidhaa feki katika bandari ya Dar es Salaam likiingizwa nchini.

Kontena hilo limesheheni bidhaa feki mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya umeme, kiwi, blenda, mashine za mahesabu na antena.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam hivi karibuni , Mkurugenzi wa Tume hiyo, Bw. Godfrey Mkocha amesema kukamatwa kwa kontena hilo ni mwanzo rasmi wa kazi ya tume yake ambayo imedhamiria kukomesha biashara ya bidhaa feki nchini.

”Tume yangu imeanza kushughulikia suala hili rasmi, kwa kuanzia tayari tumekamata kontena moja bandarini likiwa limejaa bidhaa feki”, akasema Bw. Mkocha.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nje ya nchi kuacha kuingiza bidhaa feki kwani nafasi hiyo sasa haipo na wasitegemee kuwa biashara hiyo itaendelea kuwalipa.

Amesema tume yake imejipanga vizuri katika maeneo yote ya mipakani na bandarini kuhakikisha inadaka bidhaa zote feki zinazoingizwa nchini.

Amesema FCC imeamua kwanza kupambana na wafanya biashara wakubwa wa bidhaa feki badala ya kwenda kufukuzana na Wamachinga mitaani ambao ndio wanaofikisha bidhaa hizo kwa watumiaji.

”Machinga sisi hatutamgusa, tunataka kwanza tupambane na wafanyabiashara wakubwa wa biashara hii, tukiwadhibiti hao, Machinga watakwisha wenyewe,” akasema.

Bw. Mkocha ameongeza kuwa ili kuhakikisha vita dhidi ya bidhaa feki inafanikiwa, Serikali imeunda kikosi cha kazi cha kupambana na bidhaa hizo hapa nchini.

Amesema kikosi hicho kinaundwa na wajumbe ambao ni polisi, ofisi ya Mwanasheria Mkuu, tume ya kudhibiti rushwa, shirika la viwango,TBS, Mamlaka ya Mapato Tanzania, na tume ya kudhibiti chakula na dawa.

Amesema biashara ya bidhaa feki ni uhalifu kama ilivyo kwa madawa ya kulevya na kwamba ina madhara makubwa kwa uchumi wa nchi.

Ameyataja baadhi ya madhara hayo kuwa ni pamoja na kuongeza gharama za biashara kwa wafanyabiashara wa bidhaa halali na kuingizwa kwa bidhaa zisizo na ubora.

Amesema tayari sheria ya bidhaa feki imeshapitishwa na Bunge na itaanza kutumika muda wowote baada ya huruma iliyotolewa ya muda wa miezi mitatu kumalizika.

Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete wakati akifungua maonyesho ya kimataifa ya biashara kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere aliagiza vyombo husika kuhakikisha gharama za uendeshaji wa biashara nchini zinapungua ili kuinua uchumi wa nchi.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.