21 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

NMB yaja na mfumo wa kisasa
 
2006-07-21 14:46:23
Na Aziz Issa

Katika kuboresha huduma zake, Benki ya NMB imeanza zoezi la kuondoa mfumo wa utunzaji wa takwimu wa zamani na kuingiza mfumo mpya.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, benki hiyo ilianza zoezi la kubadilisha mfumo huo tangu mwezi uliopita.

Imeelezwa kuwa benki hiyo pia imeshaanza kutoa huduma kwa wateja wake kwa kutumia mfumo huo mpya katika matawi 60.

Meneja Uhusiano wa benki hiyo, Bi. Shy-Rose Bhanji amekaririwa akisema kuwa matawi mengi yaliyoanza kutoa huduma kwa kutumia mfumo huo mpya yapo katika makao makuu ya mikoa.

Amesema mkakati wa benki hiyo ni kuendelea kubadilisha mfumo wa zamani ili kukamilisha matawi yote 114 ya benki hiyo nchini.

Amesema katika mfumo huo wa zamani wateja walitakiwa kusubiri taarifa zao hadi watoaji huduma waunganishwe na makao makuu.

Hata hivyo, akasema katika mfumo huo mpya hakutakuwa na kuunganishwa na makao makuu taarifa zinapohitajika.

Akasema mfumo huo mpya hautamaliza kabisa tatizo la foleni ndefu tu, bali utasaidia kuharakisha utoaji wa huduma na hivyo wateja wao watatumia muda mfupi tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanza mfumo huo.

Mbali na kubadili mfumo huo ambao unategemea uwepo wa uhakika wa mawasiliano, benki hiyo pia imekuwa ikiendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa watoaji wa huduma ndani ya benki ili waendane na mabadiliko hayo.

Pia amesema NMB imeweka malengo ya kuhakikisha inapunguza kwa kasi kubwa foleni ambapo itaingiza mfumo wa kutumia ujumbe na kutumia mashine za ATM.

NMB inamilikiwa na Serikali kwa hisa asilimia 51, huku Benki ya Rabo ya Uholanzi ikimiliki hisa asilimia 49 kwa ushirikiano na wanahisa wa NICO,TCCIA, na Benki ya Exim.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.