|
Moto wazua msiba mzito Dar
2006-07-19 14:52:36
Na Usu-Emma Sindila, Polisi Kati
Moto umezua msiba mwingine mzito Jijini Dar es Salaam baada ya kukatisha maisha ya mtoto Salome Posian,7, na kumuunguza vibaya bibi yake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow, amesema tukio hilo lilitokea eneo la Kigogo Luhanga usiku wa kuamkia jana.
Amesema wakati moto huo unaanza, Bibi. Jane Lucas ,60 na mjukuu wake, Salome walikuwa wamelala fofofo.
Akasema chanzo cha moto huo ni mshumaa uliokuwa umewashwa chumbani na kuangukia kwenye chandarua na kisha kuenea nyumba yote.
Kamanda Rwambow amesema nyumba hiyo yenye vyumba vinne ni mali ya marehemu Berege ambapo Bi. Jane alikuwa ni mmoja wa wapangaji.
Amesema moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.
Kamanda Rwambow amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati majeruhi amelazwa hospitali ya Temeke.
Katika tukio lingine, kijana Said anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 hadi 25 anadaiwa kumuua baba yake kwa kumcharanga mapanga.
Kamanda wa Polisi wa Manispaa ya Temeke Emmanuel Kandahabi, amemtaja marehemu kuwa ni Bw. Adamu Yusuph, 48, mkazi wa Mbagala Maji Matitu ambaye alikuwa ni baba wa kambo wa kijana huyo.
Amesema hata hivyo kijana huyo amelala mbele baada ya kufanya mauaji hayo na polisi wanamtafuta.
Kamanda Kandihabi amesema chanzo cha tukio hilo ni mzozo ulifuatia baba kumuonya mwanae kutokana na tabia yake ya kurejea nyumbani akiwa mbwii kwa pombe.
Amesema wakati ugomvi huo ukiendelea, baadhi ya majirani walifika na kujaribu kuamua, lakini kijana huyo alikataa suluhu huku akisema sitaki kuamuliwa na mtu kwani nimechokozwa na baba huyu.
Amesema mtoto huyo alimkata kata mapanga baba yake huyo na watu walipoanza kukusanyika akatimua mbio na kwenda kusikojulikana.
Amesema marehemu aliyefariki wakati akiwa njiani kukimbikizwa katika Hospitali ya Temeke, mwili wake umehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika tukio lingine, watu wanne wanashikiliwa na polisi baada ya kukutwa na pombe haramu aina ya gongo.
Kamanda wa Polisi Manispaa ya Temeke Kandihabi amewataja watu hao kuwa ni Hassan Abdallah (35), Charles Madunga (26), Ahmed Sagafu (43) na Johan Samwel (37).
Akasema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
|