|
Jambazi sugu aanika siri kibao
2006-07-19 14:50:54
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Mkazi wa Jijini ambaye alitangaza rasmi kustaafu kazi ya ujambazi ameanika siri kibao kuhusu shughuli hiyo haramu.
Akiongea na gazeti hili, jamaa huyo ambaye anajulikana kwa jina maarufu la Mdudu anasema, majambazi yanapokwenda kupora siyo kwamba yanakuwa yamedhamiria kuua.
Huwa tunapenda sana kubeba tunachokitaka na kuondoka bila kumwaga damu lakini watu wanapoleta upinzani, tunalazimika kuua, anasema.
Anasema majambazi pia yana uongozi thabiti uliopangwa vizuri kama ilivyo kwenye taasisi nyingine.
Kila mmoja anatakiwa atekeleze kazi aliyopangiwa tena kwa ukamilifu na bila kufanya makosa.
Ukiharibu kazi na kusababisha dili kufichuka , lazima wenzako wakuadhibu...ndiyo maana unasikia majambazi yamepigana yenyewe kwa yenyewe ama yameuana, anasema.
Anasema kama ilivyo katika kazi nyingine, katika ujambazi pia kuna kuzidiana kete.
Wanyonge mara nyingi hunyanyaswa. Kazi kubwa ya kupora wanaifanya wao lakini huambulia dau dogo, anasema.
Anasema ukitaka kuinjoi katika ujambazi uwe kiongozi.
Wewe kuuawa si rahisi. Unatoa maagizo na wadogo zako wa kazi ndio wanaingia mzigoni, anasema.
Hata hivyo anasema katika kipindi alichokuwa jambazi, yeye hakuwa bosi hivyo aliipata freshi kwa kupigwa na wananchi wenye hasira, kudakwa na polisi.
Si unaniona usoni? Sitamaniki. Mwili mzima umejaa makovu na pia nimepata vilema vya maisha kutokana na kipigo cha wananchi wenye hasira, anasema.
Simulizi hii itaendelea kesho.
|