|
Wabunge walilia viwanja
2006-07-17 14:44:13
Na Mashaka Mgeta, Dodoma
Waheshimiwa wabunge wameshindwa kuzuia hisia zao na kuweka bayana kuwa, wanakosa viwanja vya kujirusha wanapokuwa mjini hapa katika siku za mwisho wa wiki.
Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Samuel Sitta alipokuwa akitoa matangazo ya kawaida kwenye kikao cha Bunge la bajeti linaloendelea mjini hapa.
Mhe. Sitta akasema hatua hiyo imefikiwa na wabunge waliomfikishia kimemo wakielezea hisia zao kuhusu ukosefu wa shughuli za kustarehe maarufu kama kujirusha mjini Dodoma.
Wabunge hao ambao hata hivyo majina yao hayakuwekwa wazi wakasema, mji wa Dodoma umezizima kutokana na ukosefu wa burudani zinazoweza kuwapa fursa ya kujirusha hasa baada ya kazi nzito ya kujadili na kupitisha bajeti mbalimbali za Serikali.
Hata hivyo licha ya kutotaja majina ya wabunge waliomtumia kimemo hicho, Mhe. Sitta akasema kuna uwezekano mkubwa kwamba kilitoka kwa wabunge vijana.
Aidha, Mhe. Sitta akasema suala la kuushanikiza mji wa Dodoma kuwa na starehe zinazoweza kuwafanya wabunge kupata fursa ya kujirusha halipo chini ya mamlaka ya Bunge.
Lakini akasema hisia za wabunge hao zinaweza kuwa kichocheo kwa vijana wasanii kutoka ndani na nje ya Dodoma kutumia fursa hiyo kuja kufanya shughuli zao zinazoweza kukidhi kiu ya wabunge nyakati za mwisho wa wiki.
Kwa kawaida, wabunge wengi wanapenda kutumia siku za mwisho wa wiki kwa ajili ya kwenda Mnadani, eneo maarufu kwa upatikanaji wa nyama choma inayosindikizwa na vinywaji vya aina mbalimbali na hivyo kupata burudani ya kukidhi uchovu wa siku za katikati ya juma.
|