|
Risasi zarindima ndani ya bar Dar
2006-07-17 14:43:18
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Eneo moja Jijini Dar es Salaam juzi usiku liligeuka kama uwanja wa vita baada ya risasi kurindima na damu kumwagika.
Kana kwamba hiyo haitoshi, raia wasio na hatia walijikuta wakipagawa kwa hofu na kutimka bila mwelekeo huku kila mmoja akiomba Mungu amwepushe na balaa hilo.
Mambo yenyewe yalikuwa hivi:Usiku wa kuamkia juzi kwenye kama saa tano hivi, katika bar moja ijulikanayo kama Nonzo Pub iliyopo Mabibo Mpakani Jijini Dar es Salaam, wateja walikuwa wakikamua kama kawaida.
Lakini ghafla, shetani mbaya akaingia (majambazi) na kukatisha starehe yao.
Majambazi hayo yapatayo sita yaliyokuwa yamejiweka tayari tayari, ili yaweze kupora kiulaini ilibidi yatembeze risasi.
Hata hivyo Mungu aliyapiga kofi la uso na yakajikuta yamebugi stepu na kumlamba risasi mshirika wao aliyekuwa kaunta akikusanya minoti.
Kwani yalijali? Badala ya kuondoa maiti na kukatisha mpango huo haramu, majambazi hayo yaliendelea kukusanya noti na yaliporidhika, yakalala mbele huku yakiacha maiti hiyo hapo hapo.
Katika tukio hilo lililokuwa kama sinema ya kivita, majambazi hayo pia yalimjeruhi mteja mmoja aliyetajwa kwa jina la Hamis Chesco,32, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiuguza majeraha ya risasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambo majambazi hayo sita yalianza kurusha risasi ovyo ili kuwaogopesha wateja kabla ya kuanza kazi\ yao ya uporaji.
Akasema hata hivyo kinyume na matarajio yake ya kuzoa mamilioni, yalijikuta yakiambulia Sh. 150,000 tu.
Kwa mujibu wa Kamanda Jamal, mwili wa jambazi hilo umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akiongea na gazeti hili leo asubuhi Kamanda Rwambo amesema vijana wake wanaendelea na msako mkali wa kuyanasa majambazi hayo na amewataka wananchi kushirikiana na jeshi lake. Amesema hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
|