17 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Makamba njiapanda!
 
2006-07-17 14:42:29
Na Simon Mhina, Jangwani

Katibu Mkuu wa CCM, Luteni (mstaafu) Yusuf Makamba amewekwa njia panda na kile kikundi cha watu wanaoishi mabondeni hapa Jijini, kinachojiita Mshikamano wa Kujihami au MK.

Kikundi hicho kiliundwa mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya Mzee Makamba kuchimba mkwara mzito, kwamba watu waishio mabondeni, sasa wataondolewa kwa nguvu.

Mwenyekiti wa umoja huo, Bw. Juma Shinde, amesema Mzee Makamba kama kweli yuko siriasi kuhamisha watu wa mabondeni, basi aanzie ofisi na vijiwe vya CCM vilivyoko mabondeni.

Akasema kwenye mabonde mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, kuna vijiwe vyenye bendera za CCM, ofisi za CCM na wanachama wa CCM kibao.

’Kwa hiyo sasa tunamuomba akavunje vile vijiwe na kushusha bendera za CCM kwenye maeneo yote ya mabondeni,’ akalonga Mwenyekiti huyo.

Vilevile akasema wanaamini sasa Mzee Makamba amepata fursa nzuri ya kuwahamisha wana CCM wanaoishi kwenye mabonde mbalimbali ili kutoa mfano kwa wananchi wengine wanaoleta ’kibri\’ kufanya hivyo.

’Akawahamishe wanaoishi kwenye mabonde ya rushwa, uzembe na wale wanaotumia kofia za chama, kuwalipisha wananchi michango ya ovyo,’ akasema.

Mwenyekiti huyo akasema watamkumbuka Mzee Makamba kama mtu aliyewaweka roho juu, kuliko mafuriko yenyewe.

’Ndio maana tukaamua kuunda umoja baada ya kusikia eti tunahamishwa kwa nguvu, hii ina maana na makazi yetu yangebomolewa,’ akasema mwenyekiti huyo.

Bw. Sinde amemuomba Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abbas Kandoro asiwe mtoa vitisho, bali ashirikiane nao, katika kutatua tatizo hilo.

Akasema wao hawafurahii kuishi mabondeni na si wajinga wasijue janga linalowakabili, lakini hali ya maisha ndiyo imewafanya wafikie hatua hiyo.

”Makamba alituweka roho juu utadhani haya mabonde tuliyaumba sisi.” akasema.

Licha ya vijembe hivyo, Bw. Shinde amesema walipokea kwa furaha uteuzi wa Makamba kuwa Katibu Mkuu wa CCM, kwa vile ni mwanasiasa.

Akasema CCM ilichelewa kumpa Makamba cheo hicho, kwani ndicho kilimfaa tangu mwanzo na si ukuu wa Mkoa.

Umoja huo unawajumuisha wananchi wote wanaoishi mabondeni katika wilaya zote tatu za Mko wa Dar es Salaam.

Akasema wanamtakia afya njema Mzee Makamba ili amudu majukumu yake mapya aliyokabidhiwa ndani ya CCM.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.