|
Vibaka wabuni staili mpya ya kupora
2006-07-17 14:40:09
Na Badru Kimwaga, Jijini
Baada ya Jeshi la Polisi kutangaza vita dhidi ya vibaka waliotapakaa nchi nzima, wahalifu hao nao wameibuka na staili mpya ya kuwaibia watu.
Staili waitumiayo hivi sasa vibaka wa Jijini ni kumvamia raia mwema na kisha kujifanya wanamdai na kwamba wamembamba baada ya kuwakwepa kwa muda mrefu.
Vibaka hao humpora mali zake huku raia wengine wakiamini watu hao wanafahamiana na wanadaiana na mtu huyo.
Hata hivyo, baada ya kundi la vibaka hao kutoweka na kisha raia mwema kuomba msaada, ndipo watu hushtuka kuwa kumbe mwenzao kaibiwa na pengine kujeruhiwa na kashkash za vibaka hao.
Mmoja wa wahanga wa tukio hilo ni Bw. Daud Kaburu, 27, mkazi wa eneo la Magomeni Mwembechai, aliyekumbwa na staili hiyo mpya ya wizi na kupoteza vitu vyenye thamani ya maelfu.
Mmoja wa watu ambao wamekumbana na mkasa huo, Bw. Kaburu ameliambia Alasiri kuwa alikumbana na tukio hiyo majira ya saa 3.00 usiku eneo la Kimamba.
Amesema alivamiwa na vijana wanne ambao walianza kumhoji ni kwa nini amekuwa akiwazungusha kuwalipa deni lao.
Watu wale sikuwa nawajua hata kidogo, lakini walinivamia na kudai nimekuwa nikiwakwepa muda mrefu kuwalipa chao, kabla sijaanza kuhoji nikaonyeshewa kisu na kisha wawili wakawa wananisachi mifukoni, akasimulia.
Akasema wakati tukio hilo linatokea baadhi ya wapita njia na wakazi wa mitaa hiyo walikuwa wakishuhudia, lakini hawakumpa msaada kwa imani kwamba anajuana na vijana hao.
Hata hivyo, walipomaliza kunipora na kutawanyika ndipo nikapiga kelele kuomba msaada, lakini watu walishindwa kuniamini kama nilikuwa nimeibiwa, akasema Bw.Kaburu ambaye alikumbana na mkasa huu wakati akitokea kazini kwake.
Mkazi mwingine aliyekumbana na sakata hilo ni Bi. Suzana Mariki ambaye amesema naye alivamiwa na vibaka kwa staili hiyo hiyo na kuibiwa.
Hamisi Majaliwa amesema yeye aliwashtukia vibaka hao kabla ya kuibiwa.
Kufuatia usanii huo wa vibaka, wahanga hao wametoa tahadhari kwa wakazi wengine kuwa makini kabla makubwa hayajawafika.
|