|
TASAF kusapoti miradi 1,800
2006-07-17 14:38:20
Na Aziz Issa
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii,TASAF, umepanga kufadhili miradi 1,800 nchi nzima katika kipindi cha mwaka 2006/2007.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Hawa Ghasia amesema hayo Bungeni wakati akiwasilisha hotuba yake.
Amesema kuwa aina ya miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, madaraja, madarasa,zahanati, nyumba za walimu na madaktari, visima vya maji, masoko na upandaji wa miti.
Pia amesema miradi mingine itakayotekelezwa katika kipindi hicho ni ya kuongeza kipato kwa watu wa makundi maalum.
Mheshimiwa huyo amesema kwa kushirikiana na jamii, halmashauri na Ofisi ya Waziri Kiongozi kwa upande wa Unguja na Pemba zitahakikisha miradi ambayo haikukamilika katika awamu ya kwanza ya TASAF inakamilishwa.
Sambamba na hilo, amesema katika kipindi hicho mfuko huo utaendelea kujenga uwezo na uelewa wa wananchi kuhusu suala zima la utekelezaji wa miradi kwa lengo la kuwa na miradi endelevu.
Pia kuimarisha dhana umiliki wa jamii na kuifanya jamii itambue kuwa miradi hiyo ni mali yao na kwa ajili ya maendeleo yao.
Aidha, amesema mfuko huo utasimamia utaratibu unaowezesha taasisi mbalimbali kupitishia fedha TASAF kwa ajili ya malengo maalum.
Amesema utaratibu huo hadi sasa unanufaisha miradi ya Marine and Coastal Enviromental Management Programme(PFM).
|