14 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Viazi vyaleta msiba mzito
 
2006-07-14 15:54:32
Na Ally Hengo, PST, Kisarawe

Viazi vimezua msiba mzito katika kitongoji cha Bombani, Pugu Mwakanga baada ya kuua watu wawili kwa siku moja.

Mbali na hao waliopoteza maisha pia wengine wawili wamelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Ilala ya Amana wakiwa katika hali ambazo si nzuri.

Waliopoteza maisha wametajwa kuwa ni mtoto Filomena Joseph mwenye umri wa miaka miwili na mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Kulwa.

Habari kutoka kwa familia hizo zinadai kuwa viazi hivyo vilivyoua vilichimbwa na kupikwa na mama wa watoto hao juzi asubuhi .

Baba mzazi wa Filomena, Bw. Joseph Michael Kimaro amesema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi baada ya mkewe, Bi. Celina Josephat pamoja na shoga yake aliyetajwa kwa jina la Mama Kulwa kwenda kuchimba viazi hivyo na kisha kuviandaa kwa ajili ya kifungua kinywa.

Akasema aliporudi kutoka kwenye mihangaiko yake majira ya saa 6.00 mchana, alielezwa na mkewe kuwa mtoto wake Filomena amelala ndani kutokana na maumivu ya tumbo yaliyompata ghafla.

Akasema alipouliza kulikoni, alielezwa suala la viazi walivyonywea chai asubuhi.

Kwa mujibu wa bwana huyo, hali ya mtoto ilipozidi kuwa mbaya walimkimbiza kupata huduma ya kwanza katika zahanati ya MICO ya Gongolamboto na baadaye kurudi nyumbani.

Hata hivyo akasema walipofika tu nyumbani, mtoto Filomena alifariki dunia.

Akasema wakati Filo anakufa, walipata taarifa kwamba watoto wawili wa jirani yao ambao ni mapacha, nao hali zao ni mbaya.

Habari zaidi zinasema Kulwa na Dotto walikimbizwa hospitali ya Amana lakini Kulwa akafariki muda mfupi baada ya kufikishwa huko.

Mjumbe wa eneo hilo la Pugu Bombani, Bw. Alan Minja amethibitisha taarifa hizo na kusema viazi hivyo walivyochimba akinamama hao havifai kuliwa na binadamu japo vinafanana na viazi vya kawaida.

Amesema kabla ya mazishi kufanyika, alishauri taarifa zipelekwe kituo cha polisi cha Mabatini, Majumba Sita kwa vile vifo hivyo si vya kawaida.

Jana Alasiri ilishuhudia Defenda la polisi lenye namba PT 0965 likitinga nyumbani kwa Bw. Kimaro na kumhoji na kisha kuondoka na mwili wa marehemu Filomena.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.