|
Vituo vya polisi vyavunjwa usiku
2006-07-14 15:51:28
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Katika hali inayoonyesha uhalifu umevuka mipaka, huko mkoani Kilimanjaro watu wanaodhaniwa kuwa ni wezi,
wamevamia vituo vya polisi na kuvivunja na kisha kuiba vitu mbalimbali.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, Venance Tossi amevitaja vituo hivyo kuwa ni kituo cha jirani na shule ya sekondari ya Mawenzi na kile cha Kwa Mapadri.
Amesema wezi hao walisomba hadi milango na madirisha ya majengo hayo.
Amesema wizi huo ulifanyika baada ya kugunduliwa kwamba vituo hivyo vilikuwa havitumiki kwa muda mrefu na vingine hutumika nyakati za mchana.
Kamanda huyo akasema vituo hivyo vilijengwa bila kuzingatia mahitaji na taratibu za ujenzi wa vituo katika maeneo ya watu na matukio ya uhalifu.
Ameongeza kuwa yawezekana vituo hivyo vilijengwa kwa utashi wa watu wachache wenye uwezo ama sababu nyingine za kisiasa kwa malengo ya kutaka kulindiwa mali zao bila kuzingatia mahitaji halisi katika eneo husika.
Hata hivyo amesema polisi itaendelea kujenga vituo vidogo vya polisi kulingana na mahitaji ya eneo husika, idadi ya watu, matukio ya uhalifu, umbali kati ya kituo na kituo kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.
|