|
Mishahara bubu hiyo!
2006-07-14 15:50:53
Na Kiyao Hoza, Dodoma
Wabunge wa upinzani wamemjia juu Waziri katika Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) Mheshimiwa Hawa Ghasia wakimtaka aeleze wazi nyongeza ya mishahara itakuwa bei gani ili watu waweze kupanga mambo yao vizuri.
Akiwasilisha hotuba ya upinzani, Msemaji Mkuu wa kambi ya upinzani, kwa wizara hiyo, Mhe. Shoka Khamis Juma, amesema nyongeza hizo ziko kibubu bubu\.
Katika hotuba yake, Waziri Ghasia amesema mishahara ya watumishi wake itapanda kwa kiwango cha kati ya asilimia 15 hadi 50 kuanzia mwezi huu.
Hata hivyo hakusema kima cha chini cha mshahara kitakuwa kiasi gani.
Kwa mahesabu ya haraka haraka, kwa nyongeza hiyo, mtu wa kima cha chini anaweza kunyaka karibu laki nzima.
Akasema mwaka huu jumla ya shilingi milioni 1,003,882 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia mishahara, ajira mpya na upandishwaji vyeo kwa watumishi wa umma.
Akasema kiwango hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 47.22 ilikilinganishwa na kiasi cha Shilingi milioni 681,897 zilizotengwa katika kipindi cha fedha cha mwaka 2005/2006.
Aidha Waziri amesema nyongeza hiyo pia itasaidia kugharimia ajira mpya 24,689, kupandishwa vyeo kwa watumishi wenye utendaji mzuri.
Hata hivyo Waziri Ghasia amesema kutokana na maelekezo ya sera, viwango vya mishahara ya watumishi watakaopandishwa zaidi ni wataalam wa fani zote na watumishi walio katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa kauli hiyo askari polisi, wanajeshi, usalama wa taifa, madaktari na wataalam wengine ndio watakaoukata zaidi wakiwaacha watumishi wengine waliotajwa na Waziri kuwa ni wa kawaida wakiendelea kujikongoja.
Mbali na suala la mishahara, kambi ya upinzani ililivalia njuga suala la viongozi na watu maarufu nchini kwenda nje ya nchi kwa lengo la kuwatafuta madaktari bigwa wakati huduma hiyo inawezekana kufanyika hapa hapa nchini.
Viongozi wetu na watu maarufu wanakimbilia nje kufuata matibabu. Tutambue kwamba wengi wa madaktari hao wanaowafuata huko Afrika Kusini na Nairobi, ni Watanzania tuliowasomesha kwa kodi zetu, akasema Mhe. Shoka kwa niaba ya upinzani.
Akasema mbali na sekta ya afya pia katika elimu kuna hali mbaya.
Akasema ili kutatua tatizo hilo ambalo ni sugu ni wajibu wa Serikali kufanya mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwata watumishi wake kuanzia ngazi ya chini mishahara, marupurupu na posho zao kwa wakati.
Mambo mengine akasema ni suala la kodi wanazokatwa watumishi kuangaliwe upya ili hatua za kuongeza mishahara zisiendelee kuwa kiini macho tu na ziweze kuboresha maisha ya kila siku ya watumishi wa Serikali.
|