|
Meya awatwisha msalaba Machinga
2006-07-14 15:48:31
Na Simon Mhina, Mwenge
Wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo kadhaa Jijini Dar es Salaam, wamekuwa wakikwamisha juhudi za matengenezo, marekebisho na ukarabati wa miundo mbinu, zikiwemo barabara na mawasiliano, kutokana na kuvamia sehemu zisizoruhusiwa.
Hayo yamesemwa na Meya wa Manispaa ya Kinondoni,Bw. Salum Londa, alipotembelea ujenzi wa kituo cha Mwenge, ambao unaonekana kukwamishwa na wafanyabiashara hao.
Kwa kifupi, Meya Londa amedai Machinga bado ni mwiba, katika shughuli za ujenzi wa kituo hicho, kutokana na kukigeuza gulio.
Bw. Londa akasema kutokana na wafanyabiashara hao maarufu kwa jina la Machinga kuvamia maeneo mbalimbali Jijini, wataalam wanashindwa kukarabati, kutokana na msongamano.
Akasema sehemu nyingi hasa zile za barabara ambazo zimevamiwa na wafanyabiashara hao, zimekuwa na foleni kubwa ya magari, kutokana na ufinyu.
Akasema hata inapotokea mashimo kwenye barabara husika inakuwa vigumu kuweka vifaa vya kukarabati na kushindwa kufanya kazi hiyo kirahisi, kutokana na msongamano.
Sehemu nyingi msongamano, hautokani na barabara mbovu, bali hutokana na uvamizi wa wafanyabiashara hawa, ambapo hata nafasi ya magari kupishana inakuwa finyuakasema.
Akatoa mfano jinsi mafundi wa mashirika ya Posta wanavyopata taabu kwenye baadhi ya maeneo wakati wa kukarabati mikonga.
Pia akazungumzia mafundi wa DAWASA aksiema wanapata taabu wanapofanya kazi ya kubadili mabomba kutokana na msongamano wa wafanyabiashara hao.
Bw. Londa amesema kutokana na wingi wa wafanyabiashara hao, huunda umoja, ambapo inakuwa vigumu kwa mafundi hao kuwasemea mbovu.
Jamani nimekuja hapa mimi kiongozi wenu, haya mambo ya kukamatana mashati na kupigana vikumbo katika harakati za kuhamishana kwa nguvu hayana maana, tafadhalini, muondoke,akasema Bw. Londa katika kituo cha Mwenge.
Hata baada ya kituo hicho kuhamishiwa eneo la Makumbusho, wafanyabiashara hao, wamekuwa wakimiminika kila kukicha.
Awali gazeti hili lilishuhudia wafanyabiashara hao, wakikwaruzana na mafundi ujenzi ambao wanachimba mitaro katika kukamilisha ujenzi wa kituo.
Mmoja wa mafundi hao alisikika akilalamika kwamba kila wanapochimba mitaro, imekuwa ikifukiwa kutokana na pitapita ya wafanyabiashara hao.
Bw. Londa amesisitiza kwamba hata ujenzi wa kituo hicho ukikamilika Machinga hawataruhusiwa kuendesha shughuli zao hapo, kwani ni kinyume cha matumizi yaliyokusudiwa.
|