|
Mabaki ya miwa kuzalisha umeme!
2006-07-14 15:46:51
Na Aziz Issa
Kiwanda cha Katani kimeanza ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi inayotokana na mabaki ya zao hilo.
Meneja Maendeleo wa kiwanda hicho, Bw. Juma Shamte ameliambia Alasiri kuwa ujenzi huo ambao umeanza mwezi huu utakamilika baada ya miezi mitatu.
Akasema kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme Kilowati 150 ambao utawawezesha kumudu mahitaji ya kiwanda pamoja na nyumba za wafanyakazi.
Bw. Shamti amesema kuwa utafiti juu ya nishati hiyo ulianza tangu mwaka 1995 kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM).
Akasema utafiti huo ulilenga katika kupunguza kiasi cha mabaki ambacho kilikuwa hakitumiki.
Amesema mbali ya kugundua kuwa mabaki hayo yanaweza kutumika katika kuzalishia gesi hatimaye umeme, pia yanaweza kutumika kutengenezea kemikali za viwandani kama spriti, makaratasi, mbolea, madawa.
Amesema gharama za utafiti huo pamoja na ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu Dola Milioni 1.5 za Kimarekani.
Bodi ya Mkonge imetoa mamilioni ya pesa katika kuhakikisha kuwa mradi huu unafanikiwa, akasema Bw. Shamte.
Akasema kiwanda hicho kitatumia tani 35 za mabaki ya zao hilo katika kutengeneza nishati hiyo.
Hata hivyo, amesema kiasi cha mabaki tani 165 ambacho kingeweza kutumika katika uzalishaji wa umeme kitabaki kutokana na uwezo wa mtambo watakaoufunga katika kiwanda hicho.
Amesema mabaki hayo ya tani 200 kama yangetumika yote yangeweza kuzalisha umeme megawatti moja ambao ungeingizwa katika gridi ya taifa kwa ajili ya matumizi ya watu wengine.
Amefafanua kuwa utalaam wanao na Serikali iko tayari katika kuwekeza kwenye kilimo cha mkonge na kuwataka wakulima wengi zaidi kujitokeza kulima zao hilo ambalo mahitaji ya soko la dunia bado hayajatimia.
Amesema mahitaji ya soko la taifa ni tani Milioni 200 lakini Tanzania imeweza kuzalisha asilimia tano.
|