|
TBS sasa yabadili mfumo wa kukagua viwango vya chakula
2006-07-13 15:42:33
Na Mary Wejja,Jijini
Shirika la viwango nchini (TBS) limebadilisha mfumo wa kukagua viwango vya chakula kutoka mfumo wa Product Certificate System na kutumia mfumo wa Management System.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa shirika hilo, Bw.Daimon Mwakyembe wakati akifungua semina ya siku tatu iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Duniani (ISO) pamoja na Shirika la Viwanda Duniani (UNIDO).
Semina hiyo iliyofunguliwa rasmi na Mkurugenzi wa TBS imeshirikisha wafanyakazi wa TBS pamoja na wadau mbalimbali kutoka viwanda vya vyakula hapa nchini.
Bw.Mwakyembe amesema mfumo mpya utasaidia kuboresha ubora wa vyakula vya hapa nchini kwa kuwa utaanza kukagua chakula tangu kikiwa shambani hadi kinapomfikia mlaji.
Amebainisha kuwa awali shirika lilikuwa linakagua kiwango cha chakula kikiwa kimeshavunwa ili kudhibitisha kama kinafaa kutumika au hakifai lakini wameamua kutumia mfumo mpya na wa kisasa ili kuendana na mfumo wa viwango vya kimataifa.
Ameongeza kuwa shirika limeamua kutumia mfumo mpya wa kiwango cha chakula ili kuongeza ubora wa vyakula hapa nchini na kuvutia watalii wengi ambao huongezeka kulingana na mazingira mazuri ikiwemo vyakula na bidhaa mbalimbali za hapa nchini.
Watalii wakila chakula kizuri watapeleka sifa katika nchi zao, hali itayotuongezea idadi kubwa ya watalii wanaoingia hapa nchini, akasema Bw.Mwakyembe.
Naye Mkuu wa Idara ya Udhibiti Ubora, Bw.Bethuel Matemba amebainisha kuwa TBS inatarajia kutoa mafunzo kwa viwanda (10) kuhusu namna ya kuzalisha bidhaa bora.
|