13 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Bi. Harusi atoweka kimiujiza
 
2006-07-13 15:39:18
Na Aboubakary Mlawa, PST Pwani

Beatrice Charles,19, (pichani) aliyetarajia kufunga pingu za maisha hivi karibuni ametoweka katika mazingira ya kimiujiza ambayo yameifanya familia yake ihahe huku na huko kumtafuta.

Baba mzazi wa binti huyo, Mchungaji Charles Maswaga wa kanisa la Aglikana amesema binti yake huenda ametwaliwa kwa nguvu za giza.

Mchungaji huyo ambaye ni mkazi wa Kibaha Mwendapole mkoani Pwani, amesema binti yake alitoweka wakati amekwenda Jijini Dar es Salaam kufanya shopping ya harusi.

Akasema tangu Juni 30 mwaka huu, alipotoweka, hadi leo wameshindwa kujua alikopotelea licha ya kuzunguka vituo vya polisi, hospitali na hata kwenye vyumba vya maiti.

Amesema kabla ya kutoweka, alikwenda kwa mchumba wake aitwaye Joseph anayeishi Buguruni Jijini Dar es Salaam na wakaongozana madukani kufanya shopping.

Kwa mujibu wa Mshungaji Maswaga, baada ya shopping, Joseph alimsindikiza hadi kituo cha mabasi na kuhakikisha amepanda na basi limeanza safari.

Hata hivyo akasema binti huyo hakufika nyumbani kwao Kibaha na wala kwa Joseph hakurudi.

”Kwa kushirikiana na polisi tumekuwa tukimtafuta Beatrice bila mafanikio na hatujui amepatwa na mkasa gani’’, Mchungaji Maswaga akasema.

Ameongeza kuwa siku zilizopita binti yake aliwahi kupatwa na mapepo mabaya lakini alipofanyiwa maombezi, akapona.

”Inawezakana mapepo yamemtokea tena kwani yanapompanda huwa hawezi kusema wala kutambua lolote linalofanyika’’, akasema Mchungaji.

Ameomba mtu yeyote aliyemuona ama kujua taarifa zake kutoa taarifa kituo chochote cha polisi ama kuwasiliana naye kwa simu namba 0713 984264 na 0784 375232.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.