|
Mzee toka mkoani afia Dar akifuatilia matibabu ya bure
2006-07-13 15:38:30
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili
Ama kweli kifo hakina kinga, kama ilivyotokea kwa mzee mmoja toka kule Tabora ambaye amekumbwa na mauti muda mfupi baada ya kutua Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano Msaidizi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, MOI, Bw. Frank Matua mzee huyo aliyefahamika kwa jina la Lucas Magwela,78,alikumbwa na mauti hayo mara baada ya kuwasili Jijini na Basi la Saddiq Line akitokea mkoani Tabora kijiji cha Kwihara.
Amesema kutokana na vielelezo alivyokutwa navyo inaonyesha basi hilo alilipanda tarehe 23 Juni, mwaka huu na akafika katika kituo cha mabasi Ubungo siku ya pili.
Hata hivyo Bw. Matua amesema nia ya mzee huyo kuja Jijini haijafahamika licha ya vielelezo hivyo kuonyesha alikuwa amepewa msamaha wa matibabu pamoja na risiti za madawa.
Bw. Matua amesema maiti ya mzee huyo ilifikishwa hapo Juni 25 mwaka huu na hadi leo imehifadhiwa mochwari kufuatia jamaa na ndugu wa mzee huyo kutofahamika.
Yaelekea mzee huyu alikuja Jijini kwa matibabu kwa kuwa alikutwa na vielelezo vya Hospitali ambavyo alikubaliwa msamaha wa matibabu, akasema Bw. Matua.
Aidha, kwenye vielelezo hivyo kuna orodha ya majina ambayo haikuelezwa kama hao waliotajwa ni ndugu zake au la.
Katika orodha hiyo wamo Bw.Juma Pauli, Makaja Ndilu na Manasugu Alad Meshack.
Pamoja na hayo, Afisa huyo akawataka ndugu na jamaa waliopo Tabora na Jijini ambao wanahusiana na mzee huyo kufika ofisi ya MOI au wapige simu namba 0713 413098 ili wapate taarifa zaidi.
|