|
Tanzania inapoteza mamilioni kwa kukosa soko la COMESA
2006-07-13 15:37:47
Na Job Ndomba, Jijini
Imeelezwa kuwa Tanzania inapoteza mamilioni ya dola za Kimarekani kutokana na kutokuwa mwanachama wa soko la nchi wanachama wa Jumuiya ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).
Imedaiwa kuwa kwa kutokuwa wanachama, taifa linapata hasara ya dola za Kimarekani milioni 70 kila mwaka kwa kushindwa kufanya biashara katika soko hilo.
Aidha imeelezwa kuwa hatua ya kujitoa katika soko hilo imesababisha wafanyabiashara wengi wa Kitanzania kushindwa kufanya biashara katika soko hilo ukilinganisha na wale wa Kenya wanaopitisha biashara zao katika mpaka wa Tunduma.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mshauri wa Uchumi,
Bw. Afwile Mwakijungu wakati wa Semina ya wadau wa biashara nchini pamoja na taasisi ya sekta Binafsi (TPSF)iliyokuwa ikijadili mikakati ya kuishawishi Serikali ya Tanzania kurejea tena katika soko la COMESA.
Bw. Mwakijungu amesema utafiti umeonyesha ni viwanda 20 tu vya ndani vingeweza kufanya biashara za bidhaa zao na kupata kiasi hicho cha fedha kinachopotea kwa kushindwa kuwa washiriki katika soko hilo.
Aidha amesema utafiti uliofanywa mwaka 2003 na 2004 umeonyesha kuwa soko la COMESA lilikuwa linalipa zaidi ukilinganisha na lile la SADC.
Amesema takwimu za mwaka 2004 zilionesha kuwa Tanzania iliuza bidhaa zake katika soko la COMESA kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 266.8 wakati katika soko la SADC iliuza bidhaa za Dola za Kimarekani 118.4 tu.
Aidha amesema kuwa utafiti wa mwaka 2003 unaonyesha kuwa bado bidhaa zilizouzwa katika soko la COMESA zilionekana kuendelea kuongoza kwa kuuza zaidi.
Ameongeza kuwa utafiti uliofanywa katika mpaka wa Tunduma kwa kipindi cha miezi mitatu ulionyesha kuwa bidhaa zinazopelekwa katika nchi za Kongo na Zambia, nchi ya Kenya ilipeleka bidhaa nyingi zaidi za kiasi cha dola za Kimarekani milioni 13 wakati Tanzania ilipitisha bidhaa za kiasi cha dola za Kimarekani milioni moja tu.
Bw. Mwakajungu amesema kuwa Tanzania ikifungua milango ya soko hilo tena basi inaweza kuokoa hasara hiyo inayopatikana.
|