|
Polisi wamwagwa Mbezi
2006-07-13 15:36:48
Na Margaret Malisa, Pst, Pwani
Ili kuimarisha ulinzi na usalama, Jeshi la Polisi nchini limeimarisha ulinzi katika kata ya Mbezi manispaa ya Kinondoni kwa kuongeza askari 48 wa doria wa miguu na magari manne aina ya defenda.
Hatua hiyo italeta unafuu kwa wananchi kwani eneo hilo limekuwa na matukio kibao ya uporaji na mauaji hasa kwa kipindi cha hivi karibuni.
Akiongea na PST ofisini kwake jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Luis Bw. Mbaruku Masoud amesema kumwagwa kwa polisi na magari hayo kumekuja baada ya matukio ya uhalifu kuongezeka.
Bw. Mbaruku amesema baadhi ya matukio ya mauaji ya kutisha ni lile la mtu mmoja aliyechinjwa na kutobolewa macho na watu wasiojulikana huko Mbezi njia ya kwenda Goba.
Tangu askari hawa waanze kazi kumekuwa na mabadiliko kwani hata usingizi tunalala tofauti na hapo awali, akasema.
Amesema vile vijiwe vya watumiaji wa madawa na kuvuta bangi hakuna tena.
Tunashukuru Jeshi la Polisi kwa jitahada zake za kuhakikisha tuna ulinzi katika kata yetu, akasema Bw. Mbaruku.
Amesema mtaa wake umetoa ushirikiano wa kutosha kwa polisi ambapo hadi sasa maeneo nane yamesitishwa kufanya biashara kwa sababu za kiusalama.
Amesema ofisi hiyo pia imesimamia mapori yasiyosafishwa ili yafyekwe mara moja.
Aidha amesema wajenzi wameonywa waache tabia ya kurundika mafundi wengi katika miji yao kwa vile hilo linaweza kuchochea vijiwe vya madawa ya kulevya na uvutaji bangi.
Pamoja na kuwa tumepewa askari hao wa doria lakini sisi wenyewe tumeunda jeshi la sungusungu kwa ajili ya kuweka mkazo suala la ulinzi...kama kuna mtu binafisi anayetaka kuongeza nguvu anaruhusiwa kwani swala la ulinzi si la mtu mmoja ni la jamii nzima, akasema.
Ameongeza, Tunataka Mbezi ya sasa isifanane na ile ya zamani...Sasa ni ari mpya na kasi mpya, vijana wa CCM tuko kwenye vita kali ya adui anayaharibu jina la rais wetu, akasema Bw. Mbaruku.
Awali kata hiyo yenye wakazi zaidi ya elfu 3000, na yenye kituo kimoja tu cha polisi ilikuwa inakabiliwa na matukio mengi ya uvamizi na uporaji wa nyumba na sehemu za biashara.
|