|
Hatuendi soko la Nyuki ngo wachuuzi Tegeta waweka wazi
2006-07-12 15:44:10
Na Margareth Simba,Tegeta
Wafanyabiashara wa vyakula wanaoendesha shughuli zao kando kando ya barabara Bagamoyo eneo la Tegeta, wamesema hawawezi kwenda katika soko la nyuki walilopangiwa na Serikali kwa sababu eneo hilo ni gumu kibiashara.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao wamesema wanaelewa kuwa wanakaidi amri ya Serikali lakini hawana namna nyingine ya kufanya kwa sababu soko la Tegeta lipo barabarani hivyo wanapata wateja kwa wingi tofauti na soko la Nyuki.
Tunavunja sheria lakini hatumuumizi wala kumwibia mtu, uvunjaji wetu wa sheria unatuletea manufaa katika familia zetu na hata Serikali pia kwa sababu kama tukiacha kuja hapa na tusiende Nyuki idadi ya vibaka itaongezeka na tutaipa Serikali kazi nyingine, akasema Bw.Issaka Gomba.
Bw. Gombo amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia eneo hilo lakini walipaswa kuangalia kabla ya kujenga mabanda kama sehemu hiyo inaweza kuwa rahisi kufika kwa wateja.
Amesema wateja wengi wanashindwa kufika katika soko hilo kutokana na umbali na pia njia yenyewe kuwa mbaya, hali inayowafanya wao kuwavuta na kuja barabarani.
Naye Bi. Anna Mushi, amesema hapendi kukaa barabarani lakini anawajibika kufanya hivyo kwa sababu wenzake wote wamehamia hapo.
Wafanyabiashara wote wapo hapa kule Nyuki hakuna wateja ndiyo maana kila mtu amekimbilia hapa, akasema.
Akasema akifanya biashara katika eneo hilo kwa siku anaweza kuondoka na Shilingi 30,000 lakini akiwa katika soko la Nyuki hujikuta akiuza kipimo kimoja cha viazi na kuondoka na Shilingi 1,500, ambayo haiwezi kukidhi haja.
Naye Bw. Ramadhani Omary, kwa upande wake ameishauri Serikali kuweka utaratibu mzuri kwa wateja ili waweze kuwafikia kwa urahisi ikiwemo ukarabati wa njia na kuhakikisha hakuna mfanyabishara anayesogelea barabara.
Bila hivyo tutakuja hapa kila siku, maana kule hakuna faida kabisa, na sisi tunajitafutia riziki...tuna familia na ndugu wanaotugemea lazima tuhangaike, akasema.
Amesema kama Serikali inataka kweli wafanyabishara wakae katika soko la Nyuki ni vyema wakaweka mkakati hata kwa kuweka polisi katika eneo hilo ili kuwazuia wafanyabishara hao wasipange vitu barabarani.
|