|
Uagizaji wa gesi ya viyoyozi upungue
2006-07-12 15:42:46
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Katika kudhihirisha kuwa Serikali imepania kutunza mazingira, wafanyabiashara wanaoagiza kutoka nje ya nchi gesi inayotumika kwenye viyoyozi na majokofu wametakiwa kupunguza uagizaji huo kwa asilimia 85.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi Msaidizi, Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Angela Madete wakati akifungua semina ya mafunzo kwa mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu, Jijini Dar es Salaam.
Kwa wafanyabiashara wanaoagiza kutoka nje gesi aina ya CFC, Serikali inasisitiza kuwa wapunguze kiasi cha R12 wanachoagiza kwa asilimia 85, akasema Bi. Madete.
Amewataka wafanyabiashara hao kuagiza kemikali mbadala kama vile R134 , R22 au R717 ambazo hazina athari kubwa katika kuharibu mazingira.
Amesema gesi aina ya R12 inaharibu tabaka la ozoni ambalo linakinga mionzi hatari ya jua kufikia viumbe hai kwenye uso wa dunia na kusababisha magonjwa ya kansa.
Kadhalika, ofisi ya Makamu wa Rais imebeba jukumu la kutoa mafunzo ya kunasa na kulejeleza gesi kwenye viyoyozi na majokofu ili kupunguza kasi ya kuagiza na kuingiza gesi hiyo nchini.
Kwa kuanzia mafundi zaidi ya 50 kutoka mikoa ya Arusha, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar wamepewa mafunzo.
Akifungua mafunzo hayo, Bi. Madete amewataka wahandisi wote wanaohudumia viyoyozi na majokofu ambao wameshapata mafunzo ya jinsi ya kunasa na kurejelesha gesi kwenye vifaa hivyo kuwafundisha wenzao ili kueneza teknolojia hiyo.
Aidha Bi. Madete ameongeza kuwa wahandisi wengi wakijua teknolojia hiyo wataweza kusaidia kuendelea kutumika kwa vifaa hivyo lakini wakizuia uagizaji wa kemikali hizo hatari kwa mazingira kutoka nje ya nchi.
Amewataka wafanyabiashara na wahandisi wote kuwa marafiki wa tabaka la ozoni kwa kuwa msitari wa mbele kuelimisha wateja wao umuhimu wa gesi mbadala.
Mwanzoni mwa miaka ya sabini, wanasayansi walivumbua kwamba kemikali zinazotengenezwa na binadamu hujipenyeza angani na kumongonyoa tabaka la ozoni.
Uchunguzi wa angahewa tangu miaka hiyo umethibitisha kwamba tabaka la hewa la ozoni limekuwa likimongonyoka kwa kasi ya asilimia tano kila baada ya miaka 10.
|