12 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wanafunzi watembelea UWAVITA
 
2006-07-12 15:41:48
Na Daniel Mkate, Sinza

Wanafunzi 30 wa kidato cha sita kutoka shule ya Sekondari Meta ya Jijini Mbeya, wameshauriwa kutokata tamaa ya kuendelea kujiendeleza baada ya kumaliza elimu yao.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu nchini, UWAVITA, Edwin Semzaba wakati akiwakaribisha wanafunzi hao waliotembelea ofisi za umoja huo zilizopo Sinza Jijini.

Aidha, wanafunzi hao wameshauriwa kuwa na utaratibu wa kununua vitabu vya kusoma na wala si kusubiri kununua vile vinavyotumika mashuleni pekee.

Bw.Semzaba amesema lengo la safari ya wanafunzi hao ni kutembelea ofisi za UWAVITA na kufahamu mchakato mzima wa vitabu ili waweze kuhamasika na kutunga vitabu vya fasihi.

”Wamekuja kutembelea ofisi zetu ili wafahamu habari za umoja huu shughuli zote zinazofanywa na nina uhakika watakaporudi shuleni kwao Mbeya wataanzisha kijarida ambacho kitawasaidia kupata uelewa zaidi wa kutunga vitabu,” amesema.

Wanafunzi hao wakiwa sambamba na walimu wawili, walipewa nafasi ya kuuliza maswali ambayo yatahamasisha kuwa waandishi bora wa vitabu nchini.

Naye Afisa Mtendaji wa Uwavita, Bw.Abbas Mkuwaje, amesema umoja wake unaangalia nafasi ya fasihi katika kuiburudisha na kuielimisha jamii, hivyo wanafunzi hao watakapoingia kwenye fani lazima waelewe hivyo.

”Tunaamini ziara yenu imelenga kujifunza kwa vitendo pamoja na kukutana na waandishi wa vitabu teule vya fasihi ya Kiswahili hususani vile vinavyotumika mashuleni,” amesema Mkuwaje.

Akizungumza katika mapokezi yao, mkuu wa msafara ambaye ni mwalimu wa shule hiyo, Bw. Rashid Mtindwa, amewashukuru Uwavita kwa kufanikisha safari yao pamoja na mapokezi.

”Nina uhakika wanafunzi wataelewa vyema taarifa ya umoja huu na wengi nadhani watajiunga ili waweze kuwa waandishi bora zaidi,” akasema Mwalimu Mtindwa.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.