|
Wezi wa mafuta watia timu Buguruni
2006-07-12 15:41:00
Na Sharon Sauwa, Buguruni
Wezi wa mafuta kwenye magari makubwa yanayosafirisha bidhaa hiyo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakitesa huko Kurasini sasa wamehamia Buguruni.
Alasiri katika uchunguzi wake imebaini nyendo za wezi hao ambao mara kadhaa imewashuhudia wakiwa na mifuko ya plastiki wakifungua koki na kuchukua mafuta wakati magari hayo yanapokuwa kwenye foleni au yanaposimama kwenye taa za kuongozea magari barabarani.
Vijana hao wamekuwa wakijiweka tayari na mifuko ya plastiki na mara magari hayo yanaposimama katika makutano ya Mandela na Uhuru, huyakimbilia na kufungua koki za mabomba hayo na kukinga mafuta kwa kutumia mifuko hiyo.
Usishangae dada hao ndio wameshazoea, hawaogopi hata siku moja kuiba mafuta, madereva hapa hawana ujanja, mmoja wa watu aliliambia gazeti hili baada ya kushuudia wezi hao wakifanya vitu vyao.
Vijana hao baada ya mifuko yao kujaa mafuta hufunga koki na kisha kukimbia kwenda kuhifadhi maeneo maalum.
Mmoja wa wakazi wa Jijini, Bi. Hilda Jeremia amesema kitendo hicho licha ya kuwa hatari kwa watumiaji wa barabara pia kinahatarisha maisha ya vibaka wenyewe.
Wanaweka mafuta, mengine yanamwagika barabara lakini kibaya zaidi wao wanapokuwa kazini, hawaangalii magari na wanaweza kugongwa, akasema mkazi huyo.
Amesema endapo kutatokea mtu akatupa njiti inayowaka ya kibiriti, eneo hilo yalikomwagika mafuta kunaweza kutokea mlipuko.
Naye Bw. Mwinyimvua Saleh ameliomba Jeshi la Polisi nchini kuweka doria ya kutosha ili wahusika waweze kudakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
|